KUELEKEA mchezo wa Kariakoo Dabi Jumamosi hii dhidi ya Simba, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameweka wazi kuwa licha ya kwamba anatarajia mchezo mgumu na wenye presha kubwa, lakini anaamini kikosi chake kina nafasi kubwa zaidi ya kuibuka na ushindi.
Yanga ambao ni vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 19, wanakwenda kucheza na Simba wanaoshika nafasi ya pili wakitofautiana pointi mbili. Mchezo huo utapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.
Akizungumza na Gazeti la Spoti Xtra, Kocha Nabi alisema: “Tunaendelea vizuri na maandalizi ya mchezo wetu ujao dhidi ya Simba, ni mchezo wa dabi hivyo bila shaka presha itakuwa kubwa nje na ndani ya uwanja. Tunakwenda kucheza na Simba ambayo imeimarika baada ya kuja kwa kocha mpya.
“Lakini licha ya changamoto hizo naamini tuna nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo kulinganisha na wapinzani wetu hasa kutokana na kiwango bora ambacho tumeonesha katika michezo yetu saba ya kwanza.
“Mechi hii kushinda ni muhimu sana kwetu kwa sababu itatuongezea usalama wa kubaki vinara kwenye ligi na kujiamini kutaongezeka zaidi kwa wachezaji.“Siyo rahisi kupata ushindi mbele ya Simba kwa sababu wana timu bora na wachezaji wazuri. Malengo yetu ni kuwa mabingwa msimu huu na ili tufanikiwe tunapaswa kuzifunga timu ambazo zipo kwenye mbio za ubingwa.”