Home Uncategorized SIMBA SC YABADILI GIA KWA OKWI

SIMBA SC YABADILI GIA KWA OKWI


BAADA ya hivi karibuni mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi kudaiwa kugoma kuongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia timu hiyo, sasa mambo yamekaa sawa.

Habari njema kwa mashabiki wa Simba ni kwamba Okwi ambaye sasa yupo na kikosi cha timu ya taifa ya Uganda michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) anadaiwa kukubali kuongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia Simba.

Inadaiwa Okwi anaelekea kufikia hatua hiyo baada ya kufanya mazungumzo na mmoja wa viongozi wa Simba huko nchini Misri ambaye pia aliambatana na baadhi ya Wabongo ambao ni wapenzi na mashabiki wakubwa wa timu hiyo.

Akiwa na kikosi cha Uganda, juzi Jumamosi, Okwi alikuwa Mchezaji Bora wa Mechi dhidi ya DR Congo baada ya kufunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-0.

“Okwi anaelekea kukubali kuongeza mkataba mwingine wa kuendelea kuitumikia timu yetu baada ya kufanya mazungumzo hivi karibuni na uongozi lakini pia baadhi ya wabunge ambao ni wapenzi na mashabiki wa timu yetu.

“Mazungumzo hayo yamefanyika huko nchini Misri ambako yupo na timu ya taifa ya Uganda katika Afcon. “Kwa hiyo ni matumaini yetu kuwa kama hatobadili tena msimamo wake basi muda wowote atasaini mkataba wa kuendelea kuitumikia timu yetu,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori hakupatikana kutokana na simu yake mkononi kuita tu bila ya kupokelewa kama ambavyo pia ilikuwa kwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Swedy Mkwabi.

Mbali na makubaliano hayo, inaelezwa kuwa mara baada ya kuondoka nchini, Okwi alibadili namba ya simu kwa kuwa namba aliyokuwa akiitumia awali haipatikani hadi sasa, hivyo ilikuwa ngumu kumpata kwa njia ya simu.

SOMA NA HII  SIMBA NA AZAM FC LEO NI MWENDO WA KUTAFUTA REKODI MPYA TAIFA