MABAO mawili ya Saido Ntibazonkiza katika mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu Bara, huenda yakamnyima fursa straika Heritier Makambo kuwemo kwenye kikosi cha Yanga kitakachoivaa Simba Jumamosi katika mechi ya watani wa Jadi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kiungo huyo anampa kibarua kigumu Makambo cha kumshawishi Kocha Nasreddine Nabi kumjumuisha katika kikosi cha mechi ya watani kutokana na mahitaji ya kikanuni kwa Ligi Kuu msimu huu.
Kanuni za ligi hiyo msimu huu zinalazimisha kila timu kutumia wachezaji nane tu wa kigeni katika mchezo mmoja jambo ambalo litailazimu Yanga kuwaweka jukwaani nyota wake wawili kwani ina kikosi chenye wachezaji 10 wa kigeni.
Hata hivyo, tayari mchezaji mmoja, Yacouba Sogne atakosekana kwani ni majeruhi hivyo kati ya tisa waliobakia Yanga italazimika kumweka jukwaani mchezaji mmoja.
Katika hao tisa, Makambo ndiye anaonekana kuwa katika wakati mgumu zaidi kwani ndiye mchezaji wa kigeni ambaye kwa siku za hivi karibuni ameonekana kutokuwa na kiwango bora kulinganisha na wengine nane.
Mchezaji huyo sio tu amekuwa hana uhakika wa nafasi katika kikosi cha Yanga, bali pia hata pale anapopewa fursa ya kucheza katika mechi za Ligi Kuu, ameonekana kuwa na ukame wa kufumania nyavu kulinganisha na Fiston Mayele ambaye ndiye chaguo la kwanza la Yanga nafasi ya straika wa kati.
Ugumu wa Makambo kuwemo kikosi cha mechi ya Jumamosi unaongezeka zaidi na mwendelezo wa kufumania nyavu na kiwango bora ambacho Saido amekuwa akikionyesha kwa mechi za hivi karibuni.
Awali Saido ndiye ambaye alikuwa akitolewa sadaka ya kukaa jukwaani mara kwa mara lakini katika siku za hivi karibuni amegeuka lulu katika kikosi cha Yanga kwa kuwafungia mabao mawili katika mechi mbili tofauti walizocheza na Namungo na mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza.
Kikwazo kingine cha wachezaji hao ni ushindani wa namba katika nafasi wanazocheza ambapo wachezaji kama Djigui Diarra, Shaban Djuma, Khalid Aucho, Yanick Bangala, Jesus Moloko na Fiston Mayele kwenye mechi za hivi karibuni wakiwa na muunganiko bora ni dhahiri kuwa wanaweza kuwa sehemu ya mechi hiyo kwa kiasi kikubwa zaidi ya Mukoko, Saido na Makambo ambao wamekuwa sio chaguo la kwanza la Kocha mkuu Nasreddine Nabi licha ya kwamba bado kuna nafasi mbili za wageni.
Mukoko anawania namba na Bangala na Aucho ambao kwa sasa wanaonekana kuwa bora zaidi yake, Makambo anawania namba na Mayele ambaye yuko moto na mara nyingi huanza na kwa wakati mwingine amekuwa akitoka anaingia Yusuph Athuman na sio Makambo.
Saido yeye anabebwa na uwezo wa kucheza namba nyingi uwanjani akimudu kucheza kama mshambuliaji wa pili na winga lakini maeneo yake Feisal Salum, Moloko na Farid Mussa wanazimudu vyema hivyo kazi kwake ni kubwa.
Wazawa Erick Johora, Bryson David, Abdallah Shaibu, Yusuph Athuman, Deus Kaseke, Yassin Mustapha na Zawadi Mauya wana nafasi kubwa ya kukaa benchi na kutimiza idadi ya wachezaji 18 wanaohitajika kwa mechi kutokana na maeneo wanayocheza kuhitaji mtu mbadala amabo ni wao.
Hata hivyo, Nabi aliwahi kusema atawapa nafasi wachezaji watakaofanya vizuri kwenye kikosi chake kinapokuwa mazoezini.
“Mchezaji anayefanya vizuri mazoezini ndiye atapata nafasi ya kucheza kwani kwenye mechi tunaenda kufanya kile tulichokifanyia kazi mazoezini,” alisema.
Naye kiungo wa zamani wa Simba, Yanga na Stars Athuman Iddi ‘Chuji’ alisema wachezaji wote wanaocheza Yanga ni bora hivyo kocha anapaswa kuangalia ni nani wanamfaa kwenye mechi husika na kuanza nao.
“Huwa timu ina wachezaji wengi na hawawezi kucheza wote, licha ya kwamba Yanga msimu huu ina wachezaji bora na wengi ni wa kigeni lakini hawawezi kucheza wote hivyo kocha ndiye ataamua nani acheze mechi hiyo,” alisema Chuji.
Mchezaji na kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni alieleza kuwa mechi za Simba na Yanga hazitabiriki na yeyote anaweza kucheza.
“Hata hao wachezaji ni bora lakini ukumbuke mechi hizi hazitabiriki, unaweza kusema anacheza fulani, ukaona hayupo na kapangwa mwingine hivyo ndivyo inakuwa kwenye mechi za Simba na Yanga, tusubiri tuone,” alisema Kibadeni.
Yanga inaongoza Ligi ikiwa na pointi 19, baada ya kucheza mechi saba ikishinda sita na kutoa sare moja, mechi ya watani itakuwa ni raundi ya nane, inahitaji ushindi ili kuendelea kufukuzia ubingwa.