Home news WAKATI NABI AKIJITETE KWA KUCHEZESHA ‘FULL’ KIKOSI…KOCHA IHEFU ADAI ALITUMIA WACHEZAJI WASIOPATA...

WAKATI NABI AKIJITETE KWA KUCHEZESHA ‘FULL’ KIKOSI…KOCHA IHEFU ADAI ALITUMIA WACHEZAJI WASIOPATA NAFASI…


KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema hakuna mchezaji yoyote ambaye ni ‘staa’ ndani ya timu hiyo na aliamua kupanga ‘kikosi kamili’ katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Ihefu SC kwa sababu hakuwadharau wapinzani hao kutoka Mbarali, Mbeya.

Yanga ilipata ushindi mnono wa mabao 4-0 na kusonga mbele katika mashindano hayo ambayo hutoa mwakilishi wa Tanzania Bara kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Nabi alisema hakutaka kubadilisha kikosi chake kwenye mechi hiyo kwa sababu aliwaheshimu Ihefu ambayo msimu uliopita ilikuwa inashiriki Ligi Kuu na ina historia ya kuwabana Yanga.

Kocha huyo alisema walijianda vizuri kwa ajili ya mchezo huo na wachezaji wake wamefanya kile alichowaelekeza mazoezini na kuwasisitiza kwamba katika timu yake hakuna mchezaji ambaye atakuwa juu na wote kuhakikisha wanapambania kutafuta matokeo.

“Ni mechi niliyojiandaa kisawasawa, sikuidharau mechi hiyo kwa sababu Ihefu ni timu nzuri na msimu uliopita ilikuwa Ligi Kuu, si timu ndogo, imeshuka daraja lakini ni timu nzuri tu.

“Yanga ni timu kubwa na hakuna staa wa timu wala mchezaji mkubwa, kila mmoja ni muhimu na atapata nafasi kulingana na mahitaji yetu ya benchi la ufundi na kulingana na timu tunayoenda kukutana nayo,” alisema Nabi.

Aliongeza baada ya kuwa na uhakika na ushindi ndipo alipoanza kubadilisha wachezaji, akiwaingiza wale ambao hawajacheza muda mrefu akiwamo, Yassin Mustapha ambaye kwa muda mrefu hajaonekana uwanjani kutokana na majeraha.

“Niliwapumzisha zaidi wachezaji ambao wametumika sana kwenye timu ya taifa na Ligi Kuu kama Dickson Job na Feisal Salum, nikawaingiza nyota ambao hawajacheza muda mrefu angalau na wao wapate muda wa kucheza, lakini ni baada ya kuwa na uhakika na ushindi,” Nabi alisema.

Kuhusu, Shomari Kibwana ambaye aliumia katika mchezo dhidi ya Simba, kocha huyo amesema kutokana na majeraha yake, ataushauri uongozi kumpeleka nje ya nchi kwa ajili ya kupata matibabu bora.

Aliongeza kwa sasa wataendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi yao ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara itakayochezwa Jumapili dhidi ya Prisons.

SOMA NA HII  HUKO OLD TRAFFORD NI FEDHEA MAN U WATANDIKWA VIKALI

“Kama nilivyosema awali malengo yetu makubwa ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo yetu ya Ligi Kuu na Kombe la FA, tumevuka katika mzunguko wa nne na sasa tunaenda kujiandaa na mchezo dhidi ya Prisons,” aliongeza kocha huyo.

Naye Kocha Mkuu wa Ihefu, Zuberi Katwila, alisema ‘hakuitolea macho’ mechi hiyo kwa sababu malengo yake ni kupambana na kufanya vizuri kwenye Ligi ya Championiship ambapo wako katika nafasi ya pili kwenye msimamo.

“Tulicheza michuano hii kwa sababu ni kanuni inatulazimu na tumepangiwa na Yanga, ilibidi lazima tucheze, lakini akili yetu ipo kwenye mechi za ligi, ndicho kipaumbele chetu, nikaamua kuchezesha wachezaji ambao hawachezi ili kuwalinda wachezaji wangu tegemeo,” alisema Katwila.

EDNA LEMA AREJEA

Wakati Yanga ikiwa katika mchakato wa kunasa nyota wapya, kutoa wengine kwa mkopo, imetangaza rasmi kurejea kwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga Princess, Edna Lema.

Yanga pia inawatangazia wanachama na mashabiki wake katiba yao mpya ya mwaka 2021 iliyojadiliwa katika Mkutano Mkuu wa mwaka imesajiliwa rasmi na serikali na kukamilika huko kunaruhusu utekelezwaji wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshwaji wa klabu hiyo.

Katika taarifa yao ya jana, Yanga imesema iko kwenye mchakato wa kuwapeleka nje ya Tanzania wachezaji wao, Kibwana na Yusufu Athumani huku Fiston Mayele na Yacouba Songne afya zao zinaimarika zaidi.