SIMBA ipo mjini Bukoba kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar, huku ikiwakosa nyota wake tisa, wakiwamo Bernard Morrison na Rally Bwalya ambao kwa siku za karibuni wameonekana kuibeba timu hiyo katika mechi zao za kimashindano.
Simba iliondoka jioni ya juzi ikiwa na msafara wa watu 36 wakiwamo wachezaji 22, huku nahodha wake John Bocco akikosekana katika mchezo huo utakaopigwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Mbali na Morrison na Bwalya, wengine ni Chris Mugalu na Taddeo Lwanga ambao ni majeruhi wa muda mrefu , wengine walioachwa Dar ni; Erasto Nyoni, kipa, Jeremiah Kisubi, Israel Mwenda na Pascal Wawa.
Meneja wa timu hiyo, Patrcik Rweyemamu amesema wachezaji hao tisa wameachwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo kuwa majeruhi, kuugua na matatizo ya kifamilia, lakini jeshi lililopo Bukoba, lipo tayari kupeleka moto kwa Kagera ili kuendeleza wimbi lao la ushindi.
Simba inashika nafasi ya pili katika msimamo na kama itashinda mechi ya kesho itaiengua Yanga kwa muda, kwani itafikisha pointi 21. Yanga inayoongoza msimamo imekusanya pointi 20 kupitia mechi nane kama ilizocheza Simba.
Kukosekana kwa Bwalya na Morrison kutaipa ugumu Simba kwani nyota hao wawili kwa sasa ndio wanaoonekana kuipa uhai safu ya mbele ya timu hiyo kwa uwezo wao wa kumiliki mpira, kupiga pasi za mwisho na pia kuwavuruga wapinzani kwa vipaji walivyonavyo.