ZIKIWA zimepita siku mbili tangu kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili, uongozi wa Yanga umempa jeuri kocha mkuu wa kikosi hicho, Nasreddine Nabi baada Ya kumpa majina ya mastaa watatu kwa ajili ya kufanya maamuzi ya kumsajili mmoja wao kuchukua nafasi ya Yacouba Songne ambaye ni majeruhi.
Yacouba alifanyiwa upasuaji wa goti nchini Tunisia mwezi uliopita ambapo anatarajiwa kuwa nje ya uwanja wa kipindi cha zaidi ya miezi sita, ambapo mpaka sasa Yanga inahusishwa kwa karibu na viungo, Jean-Marc Makusu wa DC Motema Pembe na Chiko Ushindi wa TP Mazembe.
Chanzo kutoka Yanga, kimeliambia Championi Jumamosi kwamba: “Katika kumsaka mbadala wa Yacouba, uongozi umempa Kocha Nabi majina matatu achague moja, ili asajiliwe, hivyo kazi imebaki kwake.”
Akizungumza na Championi Jumamosi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mbatha alisema: “Tunaridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na Kocha Nabi na benchi zima la ufundi.
“Dirisha la usajili limefunguliwa, tunafanyia kazi mapendekezo yake ili kuhakikisha tunakuwa na kikosi imara zaidi na kutimiza malengo ya kushinda ubingwa msimu huu.”
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Mwenyekiti wa Mashindano wa Yanga, Rodgers Gumbo alisema: “Nguvu kubwa katika dirisha dogo la usajili ni kuhakikisha tunatafuta mbadala wa Yacouba ambaye anatarajia kukosekana kwa msimu mzima.”
Kama Yanga itafanikisha usajili wa nyota wakali wanaotajwa kipindi hiki, basi patachimbika katika kikosi hicho kutokana na ushindani wa namna kuongezeka, huku wapinzani wakipata tabu.