Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga ni kwamba endapo Azam itatangaza leo kuachana na wachezaji wake watatu waliowasimamisha kwa madai ya utovu wa nidhamu, basi watambeba jumla kiungo fundi Salum Abubakar ‘Sure boy’.
Sure boy amesimamishwa na klabu yake sambamba na kiungo mwenzake mkabaji Mudathir Yahaya sambamba na beki mkongwe na nahodha wao mkuu, Aggrey Morris.
Hata hivyo, inafahamika kwamba wachezaji hao wameishtaki klabu yao kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufuatia adhabu yao ya kusimamishwa kwa muda usiojulikana.
Sure boy amefanya vikao sio chini ya mara mbili na mabosi wa Yanga kabla ya kukubali mkataba wa miaka miwili akisaini kimyakimya huku akisubiri hatima yake ndani ya Azam
Ndani ya Azam kulifanyika kikao kizito katika kuwajadili wachezaji hao lakini mabosi waliweka ngumu wachezaji hao kurejeshwa wakihofia kutibua zaidi nidhamu kwa wachezaji waliosalia.
Yanga wakimnasa Sure boy itakuwa ni kama wamemchukua kijana wao ambaye ni mtoto wa kiungo wa zamani wa timu hiyo, Abubakar Salum.
Pia Sure boy ataipa makali zaidi Yanga kutokana na ujuzi wake wa kupiga pasi za mabao – ubora ambao alikuwa akitamba nao akiwa na Azam.
NKANE NDANI
Usajili mwingine ni wa Denis Nkane winga wa Biashara United naye amebakiza hatua chache kuchukua mkataba wa miaka miwili.
Nkane amekuwa katika kiwango bora zaidi msimu huu na Yanga walikuwa katika hatua za mwisho kumalizana naye aje asaidiane na Jesus Muloko.
Kocha wa Yanga Nesreddine Nabi amethibitisha kuwa anamtaka winga huyo mzawa na alichovutiwa ni kasi yake na ubora aliouonyesha katika mechi za msimu huu hasa mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Ni mchezaji mzuri (Nkane) napenda kufanya kazi na vijana wadogo wenye juhudi kama yule. Akija hapa litakuwa jambo zuri. Kuna wakati lazima klabu kubwa kama Yanga ifikirie kuwaongezea thamani wachezaji wazawa,” alisema Nabi.
Naye mmoja wa vigogo wa timu hiyo aliyeomba kuhifadhiwa jina alilithibitisha Mwanaspoti kwamba Kamati yao ya Usajili wamepata mapendekezo kutoka kwa Kocha Nabi kwamba asajiliwe mashine nne tu katika dirisha dogo watakaochukua nafasi ya wachezaji watakaotemwa.
Mashine hizo ni wazawa watatu akiwamo Sure Boy, Nkane na mwingine aliyetakaa kutaja jina kwa madai bado wanaendelea kufanya mazungumzo naye.
Nyota mwingine anayetakiwa ni wa kigeni na kigogo huyo alisema anatokea Ivory Coast ingawa pia wanamsikilizia Chicco Ushindi anayekipiga TP Mazembe.
“Tayari tumeshamalizana na wawili wazawa na tumesaliwa nafasi mbili – moja ya mzawa na nyingine wa kigeni na anayekuja atakuwa anatoka Ivory Coast, ila subirini kwanza. Tunaendelea kuweka mambo sawa,” kilisema chanzo hicho ambacho kilithibitisha kwamba Nabi amependekeza nyota wanne akiwamo Ditram Nchimbi aliyeaga mapema watemwe kikosini katika dirisha hili.
Alisema Nabi ametaka mshambuliaji mmoja, beki wa kati mmoja na mawinga wawili akiwamo wa kutumia mguu wa kushoto ili kufukia shimo lililoachwa wazi na Yacouba Songne aliye majeruhi.
“Kwenye usajili wa kimataifa tuna nafasi mbili za kuongeza, pia klabu imekubaliana haitawaongeza wote itamuongeza huyo wa Ivory Coast ambaye tuko naye katika hatua za mwisho za mazungumzo na wazawa watatu ambao tayari wawili wamekwishasaini, bado mmoja.”
Ingawa imekuwa siri juu ya wachezaji watakaotemwa, lakini Nchimbi alishatimka na inaelezwa mwingine aliyekalia kuti kavu ni Paul Godfrey ‘Boxer’ na Adeyum Saleh ambao ni mabeki.
WASIKIE HAWA
Kaka wa Nkane (jina tunalo) alisema: “Dogo yupo katika mchakato wa mwisho kukamilisha suala lake la kwenda Yanga, si unajua hawezi kuondoka tu Biashara kutokana bado anamkataba.
“Ni suala la muda tu kuwekwa wazi lakini kila kitu kimekwenda vizuri kinacho pambaniwa wakati huu ni kukamilisha taratibu za kiusajili.”
Naye Meneja wa Biashara United, Frank Wabare alisema suala la Nkane kujiunga na Yanga watakuja kulizungumzia siku tatu au nne zinazofuata.
“Nkane ni mchezaji mzuri na muhimu katika kikosi chetu kama kuna suala la kuondoka kwenda timu kubwa kama Yanga, tutalizungumza muda sahihi baada ya kupata taarifa kamili kutoka kwa wakubwa wangu wa kazi,” alisema Wabare.
Nkane amebakisha mkataba wa mwaka mmoja na nusu katika kikosi cha Biashara United na Yanga wamekubaliana kulipa stahiki zote za msingi kwa timu hiyo.
Rekodi zinaonyesha msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara Nkane amefunga mabao mawili na kutoa pasi za mwisho tatu zilizotumiwa na wachezaji wengine kufunga mabao.
Katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu Nkane amefunga bao moja kwenye mechi ya ugenini dhidi ya FC Dikhil.
Gazeti la Mwanaspoti lilipomtafuta Nkane alisema suala hilo la kujiunga na Yanga viongozi wake ndio wanalifuatilia na baada ya kumalizika watalieleza lote kama lilivyo.
“Viongozi wangu wa Biashara United ndio wenye mamlaka ya kulizungumzia hili kwani mimi bado mchezaji wao kutokana na mkataba sijamaliza,” alisema Nkane.
Mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Dominic Salamba alisema Yanga inahitaji winga ambaye atakwenda kuingia katika kikosi cha kwanza kutokana bado pengo la Yacouba Sogne halijazibwa vizuri.
“Miongoni mwa mawinga waliokuwa katika viwango bora kwa kufunga mwenye, kutengeneza nafasi za kufunga, kupiga pasi na krosi nzuri kwa washambuliaji Nkane hilo analiweza ila mashaka sioni kama ataingia kwenye kikosi cha kwanza,” alisema Salamba.