UONGOZI wa kiungo fundi kutoka katika klabu ya DC Motema Pembe ya nchini DR Congo, Karim Kimvuid Kiekie umeweka wazi kuwa wapo kwenye mazungumzo na Simba na Yanga ambazo zinahitaji huduma ya kiungo huyo mshambuliaji.
Kiekie ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 19 ni miongoni mwa wachezaji wanaotamba nchini DR Congo ambapo akiwa katika umri huo tayari amefanikiwa kuitumikia timu ya taifa katika michuano ya CHAN iliyofanyika mwaka jana nchini Cameroon.
Pia kiungo huyo amefanikiwa kuingia katika kikosi bora cha msimu wa ligi kuu ya DR Congo huku pia akishinda tuzo ya kiungo bora wa mwaka wa ligi hiyo na mchezaji bora chipukizi wa ligi hiyo.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Meneja wa mchezaji huyo Lumingu Patrick Ntanda, ambaye anamiliki kampuni ya kumiliki wachezaji ya Vestiaire 32, inayommliki pia beki wa Simba Henock Inonga Baka, ameweka wazi kuwa yupo katika mazungumzo na Simba na Yanga ya kumtaka kiungo huyo ambayo alisema kuwa bado hayajakamilika.
“Simba na Yanga zote zinamhitaji Kiekie, nimefanya nao mazungumzo katika nyakati tofauti, Simba hii inakuwa ni mara ya tatu na kwa upande wa Yanga hii ni mara ya kwanza kufanya nao mazungumzo, kwa upande wa Simba mara zote tumekuwa tukishindwana katika makubaliano ya mambo ya msingi.
“Lakini safari hii Simba wameonekana kuja kivingine tofauti na mara zote, kwa upande wa Yanga kwa kuwa ndio mara yao ya kwanza ngoja tuone nini kitatokea lakini na wao wameonyesha nia ya kumhitaji Kiekie ambaye ukiachana na Simba na Yanga kutoka Tanzania, kuna timu nyingine ambazo zinamhitaji kutoka mataifa mengine kama Morocco na Tunisia,”alisema kiongozi huyo.