Home news KISA YANGA KUFUNGWA GOLI LA MAPEMA NA PRISONS…NABI ATOKWA POVU…ATAJA UKOMAVU…

KISA YANGA KUFUNGWA GOLI LA MAPEMA NA PRISONS…NABI ATOKWA POVU…ATAJA UKOMAVU…


HII Yanga ya mwaka huu itawaua watu kwa presha, ndio tambo za mashabiki kwenye vijiwe na mitandao ya kijamii baada ya mabingwa hao wa kihistoria kupindua meza na kushinda 2-1 ugenini dhidi ya Tanzania Prisons juzi, na sasa mastaa wa timu hiyo wamesema kwa mbinu za mwalimu Nasreddine Nabi na msaidizi wake Cedric Kaze, ndoo inaenda Jangwani.

Yanga imerejea juzi jioni ikitokea mkoani Rukwa ikipitia Mbeya, ambako walivuna ushindi wao wa nne ugenini, lakini kuna mambo mawili yamemshtua kocha wao timu hiyo huku akifichua kwamba wachezaji wake wanayataka hasa makombe.

Kocha Nabi amesema kwamba hatua ya Yanga kutokea nyuma kisha kushinda ugenini huo ni ukomavu mkubwa kwa timu yake.

Nabi alisema ushindi huo wa Prisons ambao waliupata katika mazingira magumu unathibitisha kwamba msimu huu wana kila dalili ya kuwa mabingwa.

Yanga ikitokea nyuma baada ya kutanguliwa kwa bao 1-0 ilisawazisha na hatimaye kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wanajeshi hao wa Magereza katika mchezo wa juzi uliopigwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa.

Rekodi zinaonyesha huu ulikuwa mchezo wa pili kwa Yanga kutokea nyuma kwa bao 1-0 kisha kushinda baada ya awali kutanguliwa 1-0 dhidi ya wanajeshi wengine wa Ruvu Shooting ambao baadaye waliwashushia kipigo cha mabao 3-1.

“Angalia tunatoka nyuma kwa bao moja tunapofanya makosa yetu lakini vijana wanatulia na kusawazisha na kupata bao la ushindi,” alisema Nabi.

“Hii ni ishara kwamba tuna kila kitu kuweza kuwa mabingwa msimu huu, najivunia sana wachezaji wangu na wasaidizi wangu wamewapa heshima kubwa uongozi na mashabiki wetu ambao wako na sisi kila mchezo.”

Nabi aliongeza kuwa alishtuka mara baada ya wachezaji wake kusimama imara wakizuia taratibu zote za kuahirisha mchezo kufuatia idadi ya wachezaji wake nane kuugua mafua makali, kichwa na kukohoa lakini bado walicheza mechi na kuibuka na ushindi.

Nabi alisema kuugua kwa wachezaji wake kulianza kabla ya safari yao ya kutokea Dar na kulazimika kumwacha staa wao Yannick Bangala ambaye hali yake ilikuwa mbaya.

SOMA NA HII  ENG HERSI NI MAFYA AISEE...KATUA CONGO KIMYA KIMYA KUMALIZANA NA MASHINE HII YA KAZI...

“Tuliugua kabla hatujaondoka Dar es Salaam hata Bangala tulimrudisha Uwanja wa Ndege akapumzike wapo pia wengine walionyesha kuvumilia tu,” alisema.

“Tulipokuwa tunaenda kwenye kikao cha mchezo idadi ya wagonjwa iliongezeka zaidi, ilinitisha sana na viongozi walianza kuchukua hatua za kuangalia kama mchezo unaweza kusogezwa mbele,” alisema.

Nabi aliwataja wachezaji waliokumbana na maradhi hayo kuwa ni kipa Diarra Djigui, mabeki Djuma Shabani, nahodha mkuu Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, viungo Mukoko Tonombe, Feisal Salum na mshambuliaji Fiston Mayele ambao wote walicheza mchezo huo kwa nyakati tofauti.

“Wachezaji waliposikia walinifuata na kukataa wakasema watacheza hawataki kusogeza mechi mbele, kama kocha lazima utashtuka lakini angalia walivyopambana.

“Huu ni ukomavu mkubwa kwa wachezaji hawa hii pia inaonyesha kwamba wako tayari kwa vita ya ubingwa kwa mazingira yoyote.”

Mayele, Fei, Aucho ni kati ya wachezaji waliokuwa mstari wa mbele kuhakikisha mechi hiyo haisogezwi mbele wakisema kuwa wana jambo lao msimu huu.