BAADA ya kuwa na mapumziko mafupi ya siku moja na nusu, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco ameweka wazi kuwa ameandaa program ya siku tano sawa na saa 120 kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Azam.
Kikosi cha Simba kilirejea rasmi Dar es Salaam juzi Jumamosi kutokea mkoani Tabora ambapo walikuwa na kibarua cha mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, ambao Simba waliibuka na ushindi wa mabao 4-1, baada ya kufika wakapewa mapumziko ya siku moja na nusu na walitarajia kuripoti kambini juzi Jumatatu.
Simba ambao mpaka sasa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wanakamatia nafasi ya pili na pointi zao 21 walizokusanya kwenye michezo tisa, Jumamosi hii wanatarajia kuwakaribisha Azam katika mchezo wa ligi utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza hivi karibuni Kocha Pablo alisema: “Kikosi kipo katika hali nzuri hasa baada ya kushinda mchezo wetu uliopita dhidi ya KMC, tuliwapa mapumziko ya siku moja na nusu wachezaji wote kwa ajili ya kwenda kujumuika na familia zao kwenye sherehe za Krismasi.
“Tupo kambini tangu Jumatatu, kwa ajili ya program za mchezo wetu ujao dhidi ya Azam ambao tutacheza Januari Mosi, tukiwa na malengo makubwa ya kuendeleza wimbi la ushindi.”