Home Makala HUYU HAPA NAHODHA WA TP MAZEMBE ALIYEAMUA KUJA KUCHEZA LIGI DARAJA LA...

HUYU HAPA NAHODHA WA TP MAZEMBE ALIYEAMUA KUJA KUCHEZA LIGI DARAJA LA KWANZA BONGO…


BILA shaka huyu ni mmoja kati ya wachezaji wenye wasifu mkubwa zaidi hapa nchini ukilinganisha na wachezaji wengine kutokana na timu alizopitia na mafanikio aliyopata.

Tunamzungumiza Yannick Bazola, mchezaji ambaye alikiwasha akiwa na TP Mazembe ya DR Congo na kupata mafanikio huku akicheza mara kadhaa Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho barani humu.

Pia aliwahi kukivaa kitambaa cha unahodha cha TP Mazembe na sasa anakipiga katika timu ya DTB akitokea DR Congo huku usajili wake unatazamwa kuwa mzuri uliofanywa na timu hiyo.

Bazola anayecheza nafasi ya kiungo amelimbia Mwanaspoti kuwa lengo la kuja nchini ni kuonyesha ubora na kiwango, na anaamini atafanya vizuri msimu huu.

“Nimekuwa na maandalizi mazuri kabla ya msimu kuanza kwani najua ili mchezaji uwe na msimu mzuri, basi unahitajika kujiandaa vyema zaidi,” anasema.

“Haijanipa shida kuja kucheza hapa nchini tena ligi ya Championship kwani niliangalia malengo ya DTB nikaona naweza kuja kuongeza nguvu zaida na hata kufanikisha hayo malengo.”

Amtaja Tabwe

Bazola anasema kuwa anavutiwa na kiwango anachokionyesha nahodha wake, Amis Tambwe katika safu ya ushambulaji na kwamba akiendelea hivyo anaweza kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo.

“Pongezi kwake kwani ameanza msimu vizuri na pia naweza kusema kuwa ni mshambuliaji ambaye muda wowote anaweza kukufunga na inakupaswa kuwa na akili kumkaba,” anasema.

“Ukiwa kiungo halafu una straika aina ya Tambwe katika pasi tatu za bao utazopiga moja inaweza kuzaa matunda kwani ni hatari akiwa analiangalia lango.”

Championship moto

Msimu huu wachezaji, makocha pamoja na wadau wanakiri Ligi ya Championship kuwa ngumu na ndivyo ilivyo pia kwa Bazola kwani anasema ina ushindani mkubwa ingawa wanaongoza ligi.

“Kila timu inaonyesha kutaka ushindi na wala hamna timu iliyoonyesha unyonge, hivyo inachangia ligi kuwa ya ushindani zaidi na kuongeza ugumu.”

Samatta ni levo nyingine

Bazola anamzungumzia nahodha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta baada ya kucheza naye misimu miwili mitatu wakiwa TP Mazembe msimu wa 2012-2013, 2014-15 na 2015-16 kabla ya kutimkia Progresso ya nchini Angola na kusema straika huyo yupo levo nyingine.

SOMA NA HII  EDO KUMWEMBE - SIMBA WAKIDHARAU IMEKULA KWAO...MANULA ANAPENDA KULALAMIKA SANA...

“Ni mmoja kati ya wachezaji wa kipekee niliowahi kuwaona na sifa zake zilitapakaa Congo kutokana na kiwango bora alichokionyesha ndani ya uwanja na hata nje ya uwanja alionyesha nidhamu kubwa,” anasema Bazola.

“Kitendo cha kunga’ra mbele ya wachezaji nyota wa TP Mazembe ilikuwa sio jambo dogo na hata alipotangazwa kuwa mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani wala sikushangaa kwani alikuwa na msimu mzuri.

“Juhudi na kujituma ndizo sifa zake na ndio sababu amefika kule aliko sasa ukitofautisha na wachezaji wengi aliokuwa akicheza nao Congo.”

Awazungumzia kina Mayele

Uwepo wa idadi kubwa ya wachezeji wa DR Congo kwenye timu kubwa nchini hasa Yanga ambayo msimu huu imewaongeza kina Djuma Shabani, Jesus Moloko, Fiston Mayele, Yannick Bangala na Heritier Makambo kumemfanya Bazola afunguke na kusema soka la Tanzania ni kubwa.

“Wachezaji wengi wa Kikongo ni gharama na wengi wao wana viwango vikubwa, hivyo ukiona nchini mwako ni kwamba ligi hiyo ni kubwa,” anasema.

“Pia nayo ni sababu ya mimi kukubali kuja huku kwani kuna wenzangu tayari wameshaweka misingi na kufanya vizuri kwenye timu zao kitu ambacho kitanifanya nisiwe mpweke sana.”