Home news MORRISON NA MKASA WA MTENGENEZA DUBWANA…ALISAJILIWA SIMBA KIMAFYA NA BADO AKAIFUNGA AKIWA...

MORRISON NA MKASA WA MTENGENEZA DUBWANA…ALISAJILIWA SIMBA KIMAFYA NA BADO AKAIFUNGA AKIWA YANGA…


KUNA mkasa mmoja wa muoka mikate ambaye aliamua kutumia roboti kuchochea makaa ya mawe kwenye tanuri lake.

Akaenda kiwandani kupeleka oda maalumu atengenezewe roboti kubwa sana kwa sababu alikuwa amejenga tanuri jipya kubwa lenye uwezo wa kuoka mikate mingi zaidi ya lile la zamani.

Akatengenezewa bonge la roboti lililoitwa MONSTER yaani dubwana. Dubwana ni dude kubwa lenye maguvu mengi ambalo linaweza kufanya chochote.

Mara nyingi madude kama haya huelezewa kwenye hadithi au kwenye filamu. Muoka mikate akashindwa kuliendesha, ikabidi arudi kiwandani kuomba msaada.

Akatumwa fundi aliyelitengeneza, akaja na kuliseti vizuri kwa ajili kuzoa makaa ya mawe. Likawa linayachota makaa mengi na kuyatupia kwenye tanuri.

Lakini yule fundi alijiamini sana, akawa anakaa nalo karibu wakati linachota makaa ya mawe. Muoka mikate akamshauri akae nalo mbali kwa sababu linaweza likamchota na yeye, akajibu kwa kujiamini “I created this Monster” yaani “mimi ndiye niliyelitengeneza hili dubwana.”

Siku moja akajichanganya, likamshika na kumchanganya na makaa na kumtupia kwenye tanuri. Akaungua vibaya na kupelekwa hospitali. Akiwa hoi kitandani, akasema “I created a monster that came to bite me” akimaanisha “nililitengeneza dubwana lililokuja kunidhuru.”

Ndugu fundi akafariki dunia, na ndiyo msemo wa Monster I crated ukaanza na kushika hadi leo. Jumapili ya Novemba 28, mwaka huu, Bernard Morison aliibeba Simba mabegani katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Red Arrows ya Zambia kwenye mechi ya mchujo ya Kombe la Shirikisho la Afrika.

Ushindi huo uliifanya mechi ya marudiano kule Lusaka, Zambia kuwa mwepesi kwani Red Arrows walikuwa na kibarua kigumu sana cha kupindua meza, na kiliwashinda.

Bernard Morison aliibwa na Simba kutoka Yanga kwa ujasusi mkubwa wa Andrew Paricha Chikoye, wakala wa Fifa mzaliwa na mkazi wa Lusaka Zambia.

Yaani Mzambia alilitengeneza dubwana Morrison ambalo limekuja kuidhuru Zambia. Baada ya Morrison kung’ara katika mechi chache za awali akiwa na Yanga, Simba wakatokwa udenda na kumtamani.

Yakafanyika mawasiliano na wakala wake aliyepo Ghana akasema Morrison ana mkataba wa miezi sita tu na Yanga. Habari hizi zikawa njema sana kwa Simba, wakatangaza nia ya kuwa naye papo hapo.

SOMA NA HII  MSIMU WA ZAWADI NA AVIATOR NDIO HUU HAPA....SHINDA TV INCH 55 KWA DAU LA BUREEE...

Wakala akasema hakuna shida, ila mimi siwezi kuja Tanzania. Kuna wakala mwenzangu nafanya naye kazi yupo Lusaka Zambia anaitwa Paricha.

Akawaunganisha Simba na wakala huyo, wakaongea na Morrison na kuelewana kila kitu. Jamaa akaja nchini Februari 20, 2020 kukamilisha dili. Wakati huo Yanga ilikuwa Tanga kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union uliofanyika Februari 23, 2020.

Akaongozana na viongozi watatu wa Simba wenye roho za kimafia. Walitoka Dar es Salaam saa mbili usiku na walisafiri kwa magari binafsi. Wakafika Tanga usiku wa manane. Yule wakala akaenda kukaa hoteli ileile waliyofikia Yanga.

Usiku huohuo Morrison akatoka chumbani kwake na kwenda chumba cha wakala na kusaini. Kulipokucha mmoja wa wale viongozi watatu wa Simba alikwenda kwenye hoteli ile kupata kifungua kichwa, yaani kama kuwadhihaki Yanga.

Kwa hiyo Morrison alisaini Simba Februari 21, 2020. Hata ile mechi ya watani wa jadi ya Machi 8, 2020 ambayo alifunga bao pekee la mchezo kwa mkwaju wa adhabu ndogo, tayari alikuwa ameshasaini Simba.

Kilichofuata baada ya hapo ni visa vyake kwa Yanga kama mwanamke aliyeichoka ndoa na anaitafuta talaka.

Kama siyo Paricha kulitengeneza dubwana Morrison kwa Simba, lisingeidhuru Zambia, lakini ndiyo hivyo tena, Simba wako hatua ya makundi na Tanzania ina nafasi nzuri ya kutetea nafasi zake nne za uwakilishi katika mashindano ya CAF. Kukosa kwa Zambia ndiyo kupata kwa Tanzania, lakini hii yote ni kwa msaada mkubwa wa dubwana Morrison.