SIMBA sasa ni wazi imeamua kujibu mapigo ya watani zao Klabu ya Yanga kwenye suala la usajili mara baada ya kubainika kuwa uongozi wa klabu hiyo umeshusha viungo wawili wa Nigeria, Michael Babatundeambaye ameshawahi kucheza Wydadi Casablanca ya Morocco na Etop Udoh ambao wataitumikia Simba katika michuano ya Kombe la Mapinduzi na wakifanya vizuri watasajiliwa.
Mbali na wachezaji hao pia inasemekana klabu hiyo imewaalika wachezaji wengine watatu ambao ni winga Mkenya Harrison Mwendwa, Gerson Fraga na Sharaff Shiboub kuitumikia Simba katika michuano hiyo.
Simba kupitia dirisha hili dogo haijaingiza wala kutambulisha mchezaji yeyote bali tayari wameshamuachia aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Ibrahim Ajibu ambaye amejiunga na Azam FC.
Kwa upande wa watani zao wa jadi Yanga wao tayari wameshamalizana na wachezaji wanne huku tayari wakiwa wameshatambulisha watatu ambao ni Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Abdoultwalib Mshery na Dennis Nkane.
Chanzo cha ndani kutoka katika Klabu ya Simba tayari kimesema kuwa, uongozi wa timu hiyo tayari umealika wachezaji watano ambao watakuja kuitumikia Simba katika michuano ya Kombe la Mapinduzi na kama wataonyesha viwango vizuri watasajiliwa.
“Ni kweli kuna wachezaji ambao watatua kwa ajili ya kuitumikia Simba katika michuano ya Kombe la Mapinduzi ambao wataangaliwa na benchi la ufundi kama wakifanya vizuri basi watasajiliwa moja kwa moja lakini kama benchi la ufundi halitawaelewa basi hawatasajiliwa.
“Hili jambo sio geni kwetu Simba kwani kama utakumbuka hata msimu uliopita katika michuano ya Mapinduzi tulileta wachezaji watatu kutoka Zimbabwe kwa ajili ya kufanya majaribio na mara baada ya kushindwa kulishawishi benchi la ufundi waliondoka, hivyo hata msimu huu pia tutafanya hivyo,” kilisema chanzo hicho.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Simba, Ally Shatry alipotafutwa kuzungumzia juu ya ujio wa wachezaji hao wapya alisema: “Kwa sasa siwezi kusema lolote juu ya hilo kwani nipo kwenye likizo ya kazi lakini ningekuwepo ofisini kila kitu ningekuwa na taarifa nacho.”