TETESI zinasema kuwa Klabu ya El Gouna ya nchini Misri inayoshiriki ligi kuu, imetuma ofa ya kumsajili Mukoko Tonombe ambaye mkataba wake unaelekea kuisha msimu huu ndani ya Klabu ya Yanga.
Kwa upande wa nyota huyo ameonekana kuifurahia ofa hiyo kwani ni wazi hana mpango wa kuendelea kubakia klabuni hapo kwa sababu ya hofu ya kukosa nafasi ndani ya kikosi cha kwanza.
Kama nyota huyo akikubali kujiunga na El Gouna basi hata maslahi binafsi yatakuwa makubwa zaidi ya mara mbili kwa namna anavyolipwa na Yanga.
Hivi karibuni Mukoko Tonombe alidai ya kuwa hajagoma kuongeza mkataba ila anaweza kuzungumza na klabu hiyo iwapo atahakikishiwa kucheza ndani ya kikosi cha kwanza.
Kauli yake hiyo ni ngumu kwani hakuna kocha ambaye anaweza kumtumia mchezaji ndani ya kikosi cha kwanza hali ya kuwa kuna wachezaji wenye uwezo zaidi yake. Hii ni ishara ya wazi aliyoonyesha Mukoko Tonombe kuwa hana nia tena ya kuendelea kusalia ndani ya klabu hiyo.
Ukweli ni kwamba ujio wa Yannick Bangala ndiyo umepoteza matumaini ya Mukoko Tonombe kuaminiwa na Mohamed Nasreddine Nabi ndani ya kikosi cha kwanza.
Licha ya kuwa Bangala alisajiliwa kama mlinzi wa kati, lakini ameonyesha uwezo mkubwa wa kuimudu nafasi ya kiungo mkabaji kuliko hata Mukoko Tonomne ambaye ndiye alikuwa kiungo bora kwa msimu uliopita wa ligi kuu.
Mukoko Tonombe alichukizwa sana mwanzoni mwa msimu huu baada ya klabu yake kumbania kuondoka kwenda kujiunga na klabu ya FAR Rabat inayonolewa na kocha wa zamani wa klabu ya Simba, Sven Van Debroeck.
Mukoko alibaniwa ofa hiyo na klabu yake kwa sababu alikuwa bado anamkataba na klabu yake. Toka siku hiyo Mukoko hakuwa na furaha tena akiamini timu yake haijali maslahi binafsi ya mchezaji.
Ofa hii iliyomjia mezani kutoka nchini Misri tena kwenye ligi yenye ushindani. itakuwa ngumu sana kwa nyota huyo kukataa kwani hii ni dalili ya mafanikio makubwa. Mukoko anatamani aendelee kuitwa timu ya taifa.
Kama akiendelea kukosa nafasi ndani ya kikosi cha kwanza cha Yanga, basi hata timu ya taifa itakuwa ngumu kuitwa.