DIRISHA dogo la usajili nchini, umesaliwa na siku tano kabla ya kufungwa Jumamosi hii, klabu ya Zanaco ya Zambia imevunja ukimya na kutoa kauli juu ya hatma ya mshambuliaji wao Moses Phiri anayetajwa kutakiwa na klabu kongwe nchini za Simba na Yanga.
Simba na Yanga zimekuwa zikipigana vikumbo kuwania saini ya Phiri, huku taarifa nyingine zikisema tayari ameshamalizana na Vijana wa Jangwani ili atue mwishoni mwa msimu huu na nyingine zikisisitiza kuwa jamaa atavaa uzi wa mitaa ya Msimbazi.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Zanaco, Roy Mutombo akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu jana asubuhi alikiri klabu yao imepokea ofa mbili za kutoka Simba na Yanga.
Mutombo alisema, Yanga ndio iliyokuwa ya kwanza kumtaka Phiri tangu mapema mwaka jana, lakini baadaye kasi yao ikapungua ndipo wakaibuka Simba baadaye.
“Ukweli ni kwamba tumepokea ofa mbili za kuhitajika kwa Phiri kimaandishi kutoka kwa klabu zote mbili za hapo kwenu Tanzania, yaani Simba na Yanga,” alisema Mutombo na kuongeza;
“Yanga ndio walikuwa wa kwanza na nakumbuka ilikuwa mwaka jana katikati walituandikia na tukazungumza nao ila kuna kipindi wakawa kimya kidogo. Baadaye Simba nao wakatuandikia pia kumtaka mchezaji huyohuyo, hivyo tukawa tunazungumza nao kisha wanapotea wanarudi tena hali ikawa hivyo.”
Mkurugenzi huyo akaongeza kwa kusema lakini ghafla hivi karibuni mabosi wa Yanga walirudi tena kwa nguvu katika kufufua dili hilo na bado wanaendelea kuongea nao kwa kuwa Phiri bado yuko katika mkataba.
“Yanga wamerudi tena hivi karibuni, tunaendelea kuongea nao lakini unajua mchezaji (Phiri) bado yuko katika mkataba ambao nisingependa kuweka wazi umebakiza muda gani. Tupo katikati ya msimu hapa Zambia, huyu ni mchezaji wetu muhimu na sio tu ligi unajua tupo kwenye mashindano ya CAF na muda uliobaki ukisema umuuze mchezaji halafu upate mwingine ni kama kucheza kamari ngumu kwani huwezi kujua kama utafanikiwa au la.”
Mutombo alisema kwa sasa kama viongozi wamemuachia Phiri aamue ni klabu gani anataka kusaini mkataba ili wao Zanaco wamalizane nao.
“Tumempa haki yake mchezaji naye achague upande gani anataka kucheza kama ni Yanga au Simba, akitutajia nasi tutaangalia namna ya kumalizana nayo,” alisema Mutombo, huku taarifa za uhakika kutoka Yanga zinasema tayari wameshamsainisha mkataba wa awali wa miaka miwili, ila Zanaco imewataka wamuache akipige hadi Juni ndipo itamuachia kuja Jangwani.
Yanga inamhitaji mshambuliaji anayeweza kucheza pia kama wingi ya kushoto, sifa alizonazo Phiri na Kocha Nasreddine Nabi ametoa baraka zote aletwe, kuziba pengo la Yacouba Songne aliye majeruhi, huku Simba ikitaka nyota wa kuziba nafasi ya Duncan Nyoni.