HATIMAYE Simba imefikia makubaliano mazuri na kiungo mkabaji raia wa Nigeria, Udoh Etop David na kupewa mkataba wa miaka miwili kuichezea timu hiyo.
Kiungo huyo aliletwa nchini tangu wiki iliyopita na moja kwa moja akapelekwa Unguja, Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Mnigeria huyo mara baada ya kutua Zanzibar, haraka alifanya mazoezi na timu hiyo huku akicheza mchezo wa kwanza dhidi ya Mlandege FC uliomalizika kwa suluhu na kuonesha kiwango kikubwa.
Mmoja wa mabosi wa timu hiyo, amesema kuwa, kiungo huyo aliletwa kwa ajili ya kusajiliwa moja kwa moja, lakini Kocha Mkuu, Mhispani, Pablo Franco aliomba amuangalie kwanza mazoezini na mechi za Kombe la Mapinduzi.
Bosi huyo alisema Pablo ameonekana kuvutiwa na kiungo huyo ambaye tayari amepewa mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kuichezea Simba inayojiandaa na mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Aliongeza kuwa, kusajiliwa kwa Mnigeria huyo huenda kukampa ugumu kiungo Mganda, Thadeo Lwanga kuendelea kubakia kikosini hapo.
“Dakika chache alizocheza Udoh dhidi ya Mlandege zilitosha kabisa kumshawishi Kocha Pablo kumpa mkataba wa miaka miwili.
“Kocha mwenyewe ameonekana kushawishika kumsajili kiungo huyo mwenye uwezo wa kucheza kiungo mkabaji nafasi anayocheza Kanoute (Sadio), Mkude (Jonas), Mzamiru (Yassin) na Lwanga.
“Hivyo Udoh amepitishwa na kocha, hao wengine waliokuwepo katika majaribio Shiboub (Sharraf) na Moukoro (Chekhi) huenda wakaachwa baada ya benchi la ufundi kutoridhishwa na viwango vyao,” alisema bosi huyo.
Akizungumzia usajili wa timu hiyo, Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, alisema: “Kikosi chetu kina wachezaji wengi wazuri jambo la kwanza kuna tuliowaacha ili ipatikane nafasi ya kuingiza wengine kutokana na mapendekezo ya Kocha Pablo.
“Kikubwa Wanasimba wasiwe na hofu, viongozi wao pamoja na makocha wetu tupo makini na tutawasapraizi watu kama tunavyofanya misimu mingine.
“Kutokana na mkakati tuliokuwa nao viongozi kwa kushirikiana na Kocha Pablo tunahitaji wachezaji waliokuwepo kwenye kiwango bora na kuisaidia timu wakati huu, niwatoe hofu katika usajili huu tutasajili kabla dirisha halijafungwa.”