Home news KIGOGO YANGA AFUNGUKA ALIVYOLIZWA NA SIMBA KWENYE USAJILI..AGUSIA WALIVYOLIPA KISASI CHA KIMAFIA…

KIGOGO YANGA AFUNGUKA ALIVYOLIZWA NA SIMBA KWENYE USAJILI..AGUSIA WALIVYOLIPA KISASI CHA KIMAFIA…


MWENYEKITI wa zamani wa Yanga, Imani Madega amefunguka kwa mara ya kwanza kwamba kuna usajili wa kisasi aliufanya wakati akiwa madarakani ili kuwakomoa Simba mwaka 2009.

Katika mahojiano maalumu yaliyoandikwa kweye gazeti la  Mwanaspoti mjini Chalinze, Pwani yalipo makazi yake, Madega alisema kwamba usajili wa kipa Juma Kaseja kutoka Simba kwenda Yanga ilikuwa ni kulipa kisasi.

Alisema kwamba waliamua kufanya kusudi baada ya kumkosa kiungo fundi Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye walikwenda kumnyatia mara kadhaa mazoezini.

Alisema alitumia nguvu na muda mwingi kumfuatilia Boban wakati huo, akiamini ni mchezaji mzuri ambaye angeisaidia timu yake lakini jitihada zake zilikwama.

“Nilipambana sana nilimfuatilia nakumbuka nilienda mazoezini usiku alikuwa uwanja wa shule ya Msingi Muhimbili mwaka 2009, nafika tu akayeyuka nakuja kujikuta kwenye gazeti nimeandikwa ‘Iman Madega achomeshwa mahindi, Boban atoweka’, niliumia sana kusema kweli,”alisema.

“Nilisema kabisa, nitajibu na ndipo nilipoanza jitihada za kumchukua kipenzi chao Juma Kaseja ili niwajibu na nilifanikiwa vyema kabisa kwa kutumia njia nyingi sana,”alisema Madega.

Alisema, haikuwa kazi rahisi kumpata Kaseja kutoka Simba, ilimlazimu amtumie hadi mdogo wake wa kuzaliwa Bakari maarufu ‘Beka’ ambaye alikuwa karibu na Kaseja na ndiye aliyekamilisha dili hilo mpaka kutua Yanga.

“Nilifurahi sana nakumbuka siku hiyo jioni Beka akanipigia simu baada ya kuonana na Kaseja ambaye alikuwa ni rafiki yake mkubwa, nilifurahi sana, nikakamilisha usajili wake ikiwa ni kujibu pigo la kumkosa Boban,”alisema Madega.

BOBAN/KASEJA

Madega alisema Boban ni moja ya wachezaji wazawa ambao walikuwa wakitamba na kuujua mpira na kila timu ilitamani kuwa naYe.

Kiongozi huyo anakiri kuwa Boban akiwa Simba aliisaidia sana safu ya kiungo kufanya vizuri na kuwa na ushindani mkubwa kutokana na uwezo wake mkubwa aliokuwa nao.

Kuhusu Kaseja alikiri kuwa ndiye aliyekuwa ‘Tanzania One’ wakati huo hivyo kumtoa Simba ilikuwa ni furaha kwao lakini kilio kwa Simba.

Kaseja aliposajiliwa Yanga mwaka 2009 alidumu kwa msimu huo mmoja na baadae kurejea tena Simba huku akijikuta anarudi Yanga mwaka 2013 kwa dau la sh 40 mil.

SOMA NA HII  BAADA YA KUSHINDWA KWENDA LIBYA..BIASHARA WAIBUKA NA HILI..GSM YAIKOPESHA NAULI ..

Alisema watani wa jadi Simba na Yanga raha yao pia inakuja huku kwenye sajili kwa kulizana ndio utani unazidi kunoga.

KUHUSU UBINGWA

Madega alisema hata msimu ulioisha kikosi cha Yanga kilikuwa bora, hivyo kinachotakiwa kufanyika ni viongozi kuwa makini kwa kila mchezo na wasibweteke kwa kuongoza Ligi Kuu Bara kwa pointi 29, zilizovunwa katika mechi 11 waliyocheza.

“Yanga inafurahisha na inaupiga mwingi, kama kiongozi siwezi kusifia kila kitu, kinachotakiwa ni uangalifu bila kujisahau hadi pale taji litakapotua Jangwani msimu huu,”alisema Madega na akaongeza kuwa;

“Yanga na Simba zipo kwa ajili ya ushindani, inapotokea mmoja kazubaa ama kubweteka mwingine anatumia mwanya huo kumwadhibu mwingine,ndio maana nasema Yanga msimu ulioisha haikuwa mbaya, wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wawe makini zaidi,” alisema.

Alitolea mfano wa dabi ya kwanza ya msimu huu kwamba Simba ilitumia nguvu zaidi kushindana na Yanga kutokana na kikosi walichonacho tofauti na misimu waliyochukua ubingwa.

“Yanga ilijiamini zaidi kwani wana timu imara zaidi, hivyo wao hawakutumia nguvu kama watani wao, ndio maana nasema viongozi waongeze umakini mkubwa.”