KAMA unadhani Simba, imekata tamaa ya ubingwa, kisa kudondosha pointi 11 katika mechi zao sita kati ya 12 za Ligi Kuu basi pole yako, kwani Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pablo Franco amesema vita ya ubingwa ndio kwanza imeanza.
Simba ilitema pointi mbili mbele ya Mtibwa Sugar baada ya kutoka nao sare ya 1-1 kwenye mchezo uliopigwa Manungu, Morogoro na kuifanya ifikishe jumla ya 11 ilizotema, zikitokana na sare nne na kipigo kimoja hadi sasa katika ligi hiyo.
Timu hiyo ilitoka sare na Biashara United, Yanga, Coastal Union na Mtibwa, kisha kupoteza mbele ya Mbeya City na kuifanya ipoteze jumla ya pointi 11, huku yenyewe ikivuna 25 zikitokana na mechi saba za ushindi na sare hizo nne.
Pointi ilizozitema zimeifanya iachwe kwa mbali na vinara Yanga, lakini kocha Pablo alisema Simba bado ipo kwenye mbio za ubingwa kwani ligi ndio kwanza mbichi na haoni sababu ya mashabiki wa timu hiyo kuwa na presha kwa sasa.
Kocha huyo alisema hadi sasa ligi ikiwa imechezwa raundi 13, hakuna timu yoyote iliyojihakikishia ubingwa kwa vile ligi hiyo imesaliwa na mechi nyingi kuliko zilizochezwa.
Akizungumza mara baada ya pambano lao dhidi ya Mtibwa, aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana kwenye mazingira magumu ya Uwanja wa Manungu na kuambulia suluhu ikiwa sare yao ya pili ugenini kwa msimu huu.
Ya kwanza ikiwa dhidi ya Biashara na nyingine mbili zikipatikana nyumbani mbele ya Yanga na Coastal.
Pablo alisema pamoja na changamoto ya uwanja kujaa maji na kuifanya timu ishindwe kucheza vizuri, lakini wachezaji wake walipambana na kwa sasa akili yake ni kwa michezo iliyopo mbele yao ikiwamo kiporo cha Kagera Sugar.
“Mbio za ubingwa bado nasi kama watetezi tunayo nafasi ya kuitetea, wanachama na mashabiki wa Simba wasikate tamaa kwa matokeo, ubingwa bado upo wazi na tuna mechi za kuutetea,” alisema Pablo.
“Nawapongeza sana wachezaji wangu kwa namna ambavyo walipambana kadri ya uwezo wao kupata matokeo japokuwa tumekosa pointi tatu, hata hivyo tunashukuru kwa hiyo moja,” aliongeza Pablo akizungumzia mchezo wa juzi.
“Ilikuwa ngumu sana kucheza kiufundi kutokana na hali halisi ya uwanja, ndio maana nasema wachezaji wamefanya kazi kubwa inayostahili pongezi, pamoja na hilo walitengeneza nafasi nyingi za kufunga ila kwa bahati mbaya hazikutumika vizuri,” alisisituiza kocha huyo aliyeiingia Simba makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikipangwa Kundi D na timu za Asec Mimosas ya Ivory Coast, RS Berkane ya Morocco na US Gendermarien ya Niger.
Naye kocha wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga alisema mechi yao ya juzi haikuwa nyepesi, lakini wachezaji wake walipambana ili Mtibwa isipoteze pointi zote nyumbani.
“Simba sio timu ya kuibeza, wachezaji wangu walipambana ili wasiwaangushe mashabiki wao, pointi moja sio mbaya na kwakuwa bado tuna mechi nyingi mbele tunaelekeza nguvu huku,” alisema Mayanga aliyerejea kutoka Prisons.