Kelvin John nyota ambaye alizaliwa mkoani Morogoro lakini maisha yake ya soka yalianzia jijini Mwanza katika michuano ya Umisseta. Kelvin yeye hupenda kujiita “Mbappe” kwa sasa anacheza katika klabu ya vijana ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji.
Kelvin amekuwa na maendeleo mazuri na sasa anaonekana kama ni hazina ya taifa kwa miaka ijayo. Amekuwa akiwaonesha vijana wa Kitanzania kuwa kila kitu kinawezekana.
Siku kadhaa zilizopita aliweza kufunga magoli matatu “hat trick” katika moja ya michezo ya ligi ya vijana ya nchini Ubelgiji. Mchango wa Samatta pia umesaidia sana kumuona Kelvin akicheza mpira barani Ulaya.
Mwaka uliopita jina lake lilitokea kwenye jarida kubwa akitabiliwa kama kijana atakayekuja kufanya mambo makubwa katika soka. Kuna uwezekano mkubwa Kelvin akafanya vitu vikubwa zaidi ya alivyovifanya Mbwana Ally Samatta.
Kuna wachezaji wengi wamekuwa wakipata fursa ya kwenda kucheza soka nje ya Tanzania lakini wengi wamekuwa wakishindwa kufanikiwa na kurudi nyumbani.
Lakini kwa Kelvin hali imekuwa tofauti mpaka sasa alipofikia tayari anaonekana amefanikiwa kucheza mpira barani Ulaya licha ya kuwa bado ni mapema. Mambo anayoyafanya yamekuwa pia yakiwashangaza makocha wanaye mfundisha mpira hukohuko barani Ulaya.
Kama ataendelea kuwa katika kiwango hichi katika siku zinazokuja ataitambulisha vizuri Tanzania. Tanzania ni nchi ambayo imekuwa na vipaji vingi lakini tatizo limekuwa vipaji hivi havipati fursa ya kutoka mapema kwenda katika mataifa yaliyoendelea kisoka.
Nchi za Afrika Magharibi pamoja na Afrika Kaskazini zimekuwa zikifanya vizuri kwa sababu wachezaji wao wakiwa wadogo wamekuwa wakipata fursa ya kutoka mapema kwenda kucheza mpira barani Ulaya na ndiyo maana wamekuwa na mafanikio makubwa.
Kufanikiwa kwa Kelvin John ” Mbappe” kunaweza kukafungia milango kwa vijana wengine wa Kitanzania waweze kupata nafasi ya kucheza soka barani Ulaya.
Kuna maendelea yameanza kuonekana baada ya mchezaji Mbwana Samatta kuonesha njia. Kwasasa vijana wengi wa Kitanzania wamekuwa wakiamini kuwa kucheza soka barani Ulaya katika mataifa makubwa ni jambo ambalo linawezekana.