Home news ALICHOSEMA ALLY MAYAYI KUHUSU SHABAN DJUMA…ADAI SI KILA MCHEZAJI ANAUWEZO…

ALICHOSEMA ALLY MAYAYI KUHUSU SHABAN DJUMA…ADAI SI KILA MCHEZAJI ANAUWEZO…

 


LAZIMA presha ziwapande. Ndio tambo za mashabiki wa Yanga wakimzungumzia beki wao wa kulia, Djuma Shabaan ambaye ameendelea kuonyesha moto wake, baada ya kuhusika moja kwa moja katika mabao matano, akifunga moja na kutoa asisti nne katika michuano yote, jambo lililowaibua wadau na kutarajia makubwa kutoka kwake.

Djuma, 28, aliyejiunga na Yanga msimu huu akitokea AS Vita Club ya DR Congo, alitoa asisti mbili katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Ihefu katika mechi ya Kombe la ASFC na akafunga bao lake pekee kwa penalti wakati Yanga ikishinda 3-1 dhidi ya Ruvu Shooting

Asisti zake zote mbili za Ligi Kuu zote amempa Fiston Mayele, moja katika ushindi wa 2-1 dhidi Biashara United na nyingine katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Coastal Union Mkwakwani, Tanga Jumapili iliyopita.

Wachezaji wa zamani wa Yanga, walizungumza  kwa nyakati tofauti, kuhusu kiwango cha Shabani kwamba kinaimarika siku hadi siku na miguu yake inaendelea kumwaga madini.

Mchezaji wa zamani wa timu hiyo na mchambuzi wa soka, Ally Mayay alimuelezea namna anavyoweza kuzuia, kufunga na kutoa asisti, kubwa zaidi anamuona ana mikimbio mingi uwanjani, jambo linalodhihirisha utimamu wa mwili wake na anavyojipambanua kuhakikisha timu inapata matokeo.

“Ni beki anayetambua majukumu yake bila kusukumwa, hilo ni jambo la msingi zaidi kuwa na wachezaji wa aina hiyo kwenye timu, mfano mzuri mechi ya juzi dhidi ya Coastal Union, alimsoma vyema Mayele kampa asisti ya bao,”alisema na kuogeza kuwa;

“Sio kila mchezaji ana uwezo wa kusoma mchezo na akawa na majibu ya kufanya timu inachukua pointi tatu, hivyo naona Shaban ni beki aliyeleta kitu kwenye ligi yetu,” alisema.

Naye kipa wa zamani wa timu hiyo, Benjamin Haule mtazamo wake haukutofautiana sana na wa Mayay kwani alisema soka la kisasa linahitaji aina ya uchezaji kama wa Shaban, ambaye anaweza kufanya mambo mengi uwanjani.

“Shaban anajiamini ndio maana anaweza akafunga na akatoa asisti, huku akihakikisha anaimarisha ulinzi kwa kusaidiana na kipa wake, hilo siyo jambo dogo linafanywa na beki makini zaidi,” alisema.

SOMA NA HII  ALICHOSEMA MATOLA BAADA YA ISRAEL MWENDA KUCHEZA 'FYONGO' NYINGI JANA...ATUPA LAWAMA KWA WOTE...

Andrew Tito beki wa zamani wa timu hiyo, naye hakusita kumpa heshima yake Shaban kwamba tangu ajiunge na Yanga amekuwa msaada mkubwa eneo la ulinzi.

“Kama beki hadi sasa anamiliki asisti mbili na bao moja, ujue ana kitu cha ziada, hakika Yanga ilitulia kusajili majembe ambayo yatasaidia kulinyakua taji la ligi kwa msimu huu,” alisema.

Staa huyo amekuwa miongoni mwa wachezaji wa kigeni wanaofanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara na ameitwa mara kadhaa kwenye timu yake ya Taifa ingawa huko amepoteza namba ndani ya kikosi cha kwanza.