Home news SIMBA YAMPANDISHA MZUKA KANOUTE….AAMUA KUVUNJA UKIMYA…ATANGAZA HATARI …

SIMBA YAMPANDISHA MZUKA KANOUTE….AAMUA KUVUNJA UKIMYA…ATANGAZA HATARI …

 


BAADA ya kuisaidia timu yake ya Simba kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam, huku akihusika kufunga bao la kuongoza, kiungo mkabaji wa timu hiyo kutoka Mali, Sadio Kanoute amefichua furaha aliyonayo kwa sasa na kuahidi kufanya makubwa zaidi katika kikosi hicho.

Kanoute alifunga bao lake la kwanza msimu huu na lililokuwa la kwanza pia kwa Simba kwa kichwa dakika ya 68 na kumfanya mchezaji huyo kuingia kwenye orodha ya nyota wa kigeni waliotupa kwenye Ligi Kuu Bara iliyosimama kwa muda kupisha michuano ya Mapinduzi.

Akizungumza na gazeti la  Mwanaspoti, Kanoute alisema ushirikiano mzuri anaoupata kutoka kwa wachezaji wenzake ndio siri ya ubora aliouonyesha kwenye mchezo huo kwa kupanda mbele na kuifungia timu yake bao ambalo anaamini ni kati ya michango mikubwa ndani ya timu.

“Nimeanza vizuri mwaka kwa kufunga, nilipata furaha kubwa kuwa miongoni mwa mastaa walioipambania timu kupata ushindi wa kwanza na mzuri kwa mwaka mpya wa 2022,” alisema na kuongeza kuwa;

“Nimefungua akaunti ya mabao ndani ya mwaka mpya hii ni baraka na natarajia kuwa na mwendelezo mzuri kwenye ligi na michuano mingine iliyo mbele yetu, hakuna kitu kizuri kwa mchezaji kama kufunga bao.”

Kiungo huyo mrefu, alisema mbali na ushindi walioupata kwenye mchezo huo alivutiwa na namna timu ilivyokuwa na uchu wa upambanaji kwa kila mchezaji kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mchezo huo japo walishindwa kutumia nafasi nyingi walizozipata.

“Tulicheza kwa kushirikiana kila mmoja alikuwa na uchu wa kupachika bao lengo likiwa ni moja tu kukusanya pointi tatu, ndio maana unaona nami nikifunga ingawa ni mchezaji ninayetakiwa kusaidiana na mabeki kuhakikisha haturuhusu nyavu zetu kuguswa,” alisema.

Katika mchezo huo bao la pili la Simba lilifungwa na Pape Ousmane Sakho kutoka Senegal kabla ya Mzambia Rodgers Kola wa Azam kuipatia timu yake bao la kufutia machozi kwenye mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, ukiwa wa kwanza wa ligi ndani ya 2022.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUIPELEKA YANGA MAKUNDI CAF...NABI APATA WENGE NA KIKOSI CHAKE..