Home news BAADA YA KUMTAZAMA NGUSHI MAZOEZINI..NABI AKUNA KICHWA WEE…KISHA AIBUKA NA KUSEMA HAYA…

BAADA YA KUMTAZAMA NGUSHI MAZOEZINI..NABI AKUNA KICHWA WEE…KISHA AIBUKA NA KUSEMA HAYA…


KOCHA wa Yanga, Nesreddine Nabi amezidi kuboresha makali ya kikosi chake akiendelea kugundua makali ya wachezaji na anakubali kasi ya straika wake anayefunga zaidi, Fiston Mayele, lakini ameamkua kumtega kiaina kikosini.

Kocha huyo ameshtukia staa mwingine ambaye anaamini atampa kibarua kizito Mayele na kuzidi kuifanya safu yao ya ushambuliaji iwe hatari zaidi licha ya sasa kuongoza kwa kufunga mabao mengi kuliko timu nyingine za Ligi Kuu Bara. Yanga ina mabao 23.

Nabi amemuangalia straika wake mpya, Crispin Ngushi kisha akagundua kitu flani bora na sasa ametamka kwamba atamsogeza acheze kama mshambuliaji wa kati nafasi anayotamba Mayele akisaidiwa kwa mbali na Heritier Makambo.

Kocha Nabi ameshtukia Ngushi aliyeng’ara na Mbeya Kwanza kabla ya kusajiliwa na Yanga katika dirisha dogo la Januari, kwamba jamaa anajua kufunga na kama ataendelea kumtumia kutoka pembeni kuna ubora unapungua kutoka kwake.

Akizungumza hivi karibuni, Nabi alisema anataka mshambuliaji huyo mzawa kupigania nafasi ya Mayele anayemiliki mabao sita kati ya 23 yaliyofungwa na timu hiyo katika Ligi Kuu Bara ikiwa kinara na alama zao 35.

Nabi alisema mbali na ubora wa kufunga Ngushi pia anaweza kupambana na vurugu za mabeki kutokana na kuwa na nguvu kama alivyo Mayele. “Tumekuwa tukimtumia kutokea pembeni, anafanya vizuri, lakini nimeona kuna kitu tofauti kutoka kwake, nafikiria kumsogeza pale kati awe anacheza kama Mayele kwa kuwa anaweza kufunga vizuri,” alisema Nabi.

“Ninachopenda (Ngushi) ni kijana mpambanaji ana nguvu kama Mayele za kupambana na mabeki. Nadhani kwa ujuzi wa kufunga kama akicheza pale anaweza kuwa na wakati mzuri zaidi na kuisaidia timu.”

Kocha Nabi alisema anaamini changamoto atakayoipata Mayele kwa Ngushi itamfanya awe makini zaidi uwanjani ili asiporwe namba na hiyo itaisaidia Yanga kupata mabao mengi yatakayofanikisha ndoto zao za msimu huu za kubeba ubingwa.

MSIKIE NGUSHI

Kauli hiyo ya Nabi imepokewa kwa mikono miwili na Ngushi akisema hakuna anachoweza kubisha kutoka kwa kocha wake zaidi ya kujipanga na kufanyia kazi anachotaka mkufunzi huyo.

SOMA NA HII  RASMI....MATAJIRI WAPYA LIGI KUU WAMALIZANA NA DEUS KASEKE JUMLA JUMLA...

“Kocha ndio mtu mkubwa kwangu, hivyo kama ameona kitu kutoka kwangu ninachotakiwa ni kukifanyia kazi na kujipanga kwa mabadiliko hayo na naamini yanalenga kunifanya nifanye vizuri,” alisema Ngushi. Tangu atue Yanga, Ngushi bado hajafanikiwa kuonyesha makali yake ya kufunga mabao ambapo moja ya bao lake kati ya matatu alipokuwa Mbeya Kwanza huenda likaingia katika mabao bora ya msimu huu hadi sasa likichuana na la Mayele.

Ngushi alifunga kwa ‘tikitaka’ wakati akiisawazishia Mbeya Kwanza dhidi ya Mbeya City katika mechi za awali za msimu huu, kisha Mayele kulipa alipofunga kwenye mechi dhidi ya Biashara United, vinara hao wakishinda kwa mabao 2-1.