HATA kabla haijatia mguu uwanjani kwenye mechi za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, Simba imekumbana na zali la aina yake kutoka kwa Shirikisho la Soka la Africa(CAF).
Simba ipo kundi D na timu za ASEC Mimosas ya Ivory Coast, nyumbani kwa kina Drogba, Toure, RSB Berkane ya Morocco aliko Tuisila Kisinda na USGN ya Niger.
Taarifa rasmi iliyotolewa na Asec jana, imethibitisha kwamba CAF wamewazuia kutumia Uwanja wa Robert Champroux kwa vile hauna vigezo vya ubora.
Uongozi wa klabu hiyo umeeleza pia kwamba watalazimika kuhamishia mechi zao kwenye Uwanja wa Mathieu Kerekou, uliopo Benin ambako nako huko itachezwa bila mashabiki.
Mamlaka za soka zimesema ASEC haitaweza kufanya chaguo jingine hapo Ivory Coast kwa vile hakuna uwanja mwingine unaokidhi ubora wa CAF wala Fifa.
Itakumbukwa kwamba Ivory Coast tayari imeanza kukarabati na kutengeneza viwanja vyake vyote tayari kwa kuandaa fainali zijazo za Afcon zitakazofanyika mwakani.
Ishu ya ASEC kuhamia Benin imepokewa kwa furaha na klabu za Simba na USGN kwa madai kwamba zitakuwa huru zaidi kwenye mazingira ya ugenini kuliko wangecheza Abidjan.
Vigogo wa Simba wanasema kwamba klabu hiyo kongwe huwa na fitna nyingi za nje ya uwanja ikiwa nchini kwao, hata kama hawaruhusiwi kuingiza mashabiki hivyo kucheza ugenini kutawapa Wekundu hao kujiamini zaidi.
Simba ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imejizolea umaarufu kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, inaingia Shirikisho baada ya kuteleza raundi ya kwanza ya mabingwa kwa kung’olewa na Jwaneg Galaxy ya Botswana baada ya sare ya 3-3 na kuwabeba Watswana kwa faida ya bao la ugenini.
Wawakilishi hao wa Tanzania wataanza mechi zao za makundi kwa kuwavaa Asec Jumapili ya Februari 13, jijini Dar es Salaam, wakimaliza hapo wanaenda Niger kwa USGN kisha wanaunganisha hadi Morocco kwa Berkane ya Kisinda na Florent Ibenge. Simba imepania kufanya makubwa msimu huu ili kucheza fainali ya michuano hiyo.
WAPEWA MBINU NA MASTAA
Nyota wa Simba wametakiwa kuhakikisha wanazitumia vyema dakika 45 za kwanza katika mchezo wao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya ASEC Mimosas kumaliza kazi.
Boniface Pawasa ambaye alikuwa miongoni mwa wachezaji waliokabiliana na timu hiyo mwaka 2003 wakishinda bao 1-0 nyumbani kabla ya kupoteza ugenini mabao 4-3, amesisitiza wachezaji wote wakaze mwanzo mwisho.
Alisema, anakumbuka alifunga mabao mawili katika hayo matatu waliyofunga ugenini huku katika ushindi waliotangulia kuupata nyumbani muuaji alikuwa ni winga Ulimboka Mwakingwe.
Pawasa alisema, Asec sio wa kubeza hivyo Simba inatakiwa kuhakikisha dakika 45 za kipindi cha kwanza inapata matokeo kama ambavyo ilifanya katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Dar City.
“Simba nawajua sana, wanatakiwa kupata matokeo muda huo, kinyume cha hapo mchezo utakuwa mgumu sana kwao na hasa ikizingatiwa wako kwenye uwanja wa nyumbani, wakishapata matokeo hapa nyumbani huko ugenini wataenda kupambana hata sare itakuwa vyema kwao kuliko kupoteza hapa, na ili waweze kufanya hivyo benchi la ufundi linatakiwa kuwa makini sana,” alisema Pawasa.
Alisema ASEC ni timu ambayo inamiliki akademi na ilipotea baada ya kuamini katika nyota wao chipukizi na kuachana na wazoefu.
“Kupoteza kwao miaka mitatu minne sio sababu ya kuwafanya Simba wabweteke kwa kuwa siku hizi rekodi sio kitu kabisa, wachezaji wanatakiwa kukumbuka michuano hiyo inawatangaza na wao,” alisisitiza Pawasa.