KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi, ameanza kumuandaa beki wake mpya wa kati, Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ atakayemrithi Dickson Job katika kikosi chake.
Hiyo ni baada ya Job kutumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya shilingi 500,000 kwa kosa la kumkanyaga kwenye mbavu mchezaji wa Mbeya City, Richardson Ng’ondya, jambo lililotafsiriwa kuwa ni mchezo wa hatari.
Job, mchezo wake wa kuukosa ni wa leo wa Kombe la FA dhidi ya Biashara United utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, kisha ataukosa mchezo dhidi ya Mtibwa, Februari 23, na ya mwisho ni dhidi ya Kagera Sugar Februari 27.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimepatikana kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, lililopo chini ya Nabi, Bacca haraka alianza kuandaliwa mara baada ya kupokea taarifa za Job kufungiwa.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa Bacca amepewa mbinu za aina ya uchezaji huku akicheza pacha na nahodha Bakari Mwamnyeto katika mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea Uwanja wa Avic Town, Kigamboni nje ya Dar ambako timu hiyo imepiga kambi.
Aliongeza kuwa upo uwezekano wa beki huyo kuanza katika mchezo huo dhidi ya Biashara pamoja na ule wa Ligi Kuu Bara watakaocheza na Mtibwa Sugar huko Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
“Mara baada ya benchi la ufundi kupata taarifa za Job kufungiwa kucheza michezo mitatu, haraka benchi la ufundi limeanza kumuandaa mbadala wake atakayechukua nafasi yake.
“Wapo mabeki wengi wenye uwezo wa kucheza nafasi hiyo, akiwemo Bangala (Yannick), lakini kocha anafikiria kumuanzisha Bacca katika mchezo ujao dhidi ya Biashara.
“Uzuri kocha ndiye aliyependekeza usajili wake katika dirisha dogo, hivyo atajua jinsi ya kumtumia katika michezo mitatu ijayo inayofuatia ya ligi na FA,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia hilo, Nabi alisema: “Nina kikosi kipana cha wachezaji wenye uwezo sawa, hivyo kama akikosekana mmoja, anakuwepo mwingine mwenye kiwango kikubwa, hivyo sina hofu kukosekana kwa Job.”