RASMI uongozi wa Simba umethibitisha kuachana na staa mmoja mkubwa wa kigeni katika timu hiyo ili kiungo mshambuliaji wa US Gendarmerie ya nchini Niger, Mnigeria, Victorien Adebayor achukue nafasi yake.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu uongozi wa Simba utangaze kuwepo mipango ya kumsajili Adebayor baada ya kuvutiwa na kiwango chake walipokutana kwenye mchezo wa pili wa Kundi D katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
Taarifa zinasema kuwa, mshambuliaji Mkongomani, Chris Mugalu, ndiye anayetajwa kuachwa kutokana na kuwa na matatizo mengi ikiwemo majeraha ya mara kwa mara.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema mara baada ya usajili wa Adebayor kukamilika, watalazimika kuachana na mchezaji mmoja wa kigeni.
Try Again alisema lengo ni kwa ajili ya kupata nafasi ya moja ya mchezaji wa kigeni watakayemsajili kutokana na kubanwa na kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambazo zimeruhusu kusajili wachezaji 12 wa kigeni idadi ambayo ndani ya Simba kwa sasa imekamilika.
Aliongeza kuwa, jukumu hilo la kumuacha mchezaji mmoja wa kigeni kati ya hao 12, lipo chini ya benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu, Pablo Franco.
“Muda wa usajili bado haujafikia, hivyo kocha ana nafasi ya kuangalia mchezaji gani hawezi kuendana na falsafa yake na asiye na mchango katika timu.
“Hivyo tupo katika mazungumzo mazuri na meneja wa Adebayor ambaye katika dirisha dogo alinishawishi tumsajili, lakini kanuni za wachezaji wa kigeni zikatuzuia.
“Ili tumsajili Adebayor, basi itatulazimu kumpunguza mchezaji mmoja wa kigeni, na wale tutakaowaacha ni walioshindwa kuonesha kiwango bora cha kumshawishi kocha,” alisema Try Again.
Wachezaji wa kigeni waliopo Simba kwa sasa ni Pascal Wawa, Joash Onyango, Henock Inonga, Sadio Kanoute, Taddeo Lwanga, Pape Sakho, Meddie Kagere, Chris Mugalu, Bernard Morrison, Peter Banda, Clatous Chama na Rally Bwalya.