SIMBA usiku wa leo inashuka uwanjani kuvaana na RS Berkane ya Morocco, huku mastaa wake wakipewa mchongo mzima wa kutoboa mbele ya wenyeji wao katika mechi hiyo ya Kundi D ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Nyota wa Simba wamepewa mchongo wa kuzingatia mambo matatu muhimu ili kutoboa kiulaini mbele ya Wamorocco.
Mabeki wa zamani wa kimataifa wa Tanzania waliowahi kukipiga Simba, Boniface Pawasa na George Masatu ndio waliotoa mchongo huo wakiwawataka Simba kuwa makini, kupambana na kucheza kwa nidhamu ili kuwasapraizi wenyeji wao.
Pawasa alisema; “Berkane ni timu nzuri hata Simba nao ni wazuri, ndio maana wako katika michuano hiyo, hivyo wachezaji wapambane na kujituma muda wote hata ikitokea wamefungwa au wao kufunga.”
Masatu aliyewahi kutamba na Pamba ya Mwanza alisema, katika mchezo huo safu ya ushambuliaji inatakiwa kuchangamka muda wote wa mchezo ili kupata matokeo ya mapema.
“Washambuliaji wamekuwa wakikosa umakini sana, nafasi nyingi wanazipoteza lakini ni sehemu ya mchezo hivyo basi wanatakiwa kulijua hilo maana huo mchezo ni mgumu sana kwa pande zote mbili,” alisema Masatu aliyetaka pia mashabiki wa soka nchini kujivunia uwakilishi wa Simba katika michuano hiyo kwa kuwa unaipa nchi heshima kutokana na uwakilishi wa timu nne ambao umepatikana hivi karibuni.
Simba ndio vinara wa kundi hilo lenye timu za Asec Mimosas ya Ivory Coast na US Gendermarie (USGN) ya Niger baada ya kukusanya pointi nne kupitia mechi mbili zaa awali ilizocheza, ikiilaza Asem mabao 3-1 na kutoka sare ya 1-1 na USGN, ulihali Berkane ilipoyop nafasi ya pili ikishinda 5-3 dhidi ya USGN na kupasuka kwa Asec kwa mabao 3-1.