Home Makala KISA KIFO CHA ALLY MTONI ‘SONSO…EZEKIEL KAMWAGA AWAVAA RUVU SHOOTING…AFICHUA UZEMBE ULIVYOKUWA…

KISA KIFO CHA ALLY MTONI ‘SONSO…EZEKIEL KAMWAGA AWAVAA RUVU SHOOTING…AFICHUA UZEMBE ULIVYOKUWA…


KUNA misiba lakini kuna msiba wa aliyekuwa mchezaji wa Taifa Stars, Ali Mtoni ‘Sonso’. Namaanisha nini? Namaanisha ipo misiba ambayo ikitokea unasema kazi ya Mungu haina makosa lakini sisi kama wanadamu, ni lazima wakati mwingine tuulizane maswali magumu kidogo.

Kwangu mimi, marehemu Sonso ni shujaa wa Taifa. Ni shujaa kwa sababu yeye ni sehemu ya kikosi chetu kilichofanikiwa kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Misri mwaka 2019. Hiyo ilikuwa ni takribani miaka 40 baada ya Tanzania kushiriki mashindano ya namna hiyo mwaka 1980.

Leo tunazungumzia kina Leodgar Tenga, Peter Tino, Jella Mtagwa na wengine kwa waliyoyafanya miaka 40 iliyopita. Miaka 40 inayokuja na kuendelea, tutakuwa tunazungumza kuhusu kina Mbwana Samatta, Simon Msuva na Sonso. England mpaka leo wanaimba kuhusu timu yao iliyotwaa Kombe la Dunia mwaka 1966 na karibu wapenzi wote wa soka wanajua nani wamebaki hai miongoni mwa wachezaji waliokuwa katika kikosi kile.

Baada ya kupata taarifa za kifo cha Sonso wiki iliyopita, nilifumba macho na kusali kumwombea heri. Nilipofumbua macho, nilipiga simu kwa marafiki zangu waandishi wa habari na madaktari wa michezo Tanzania kuuliza nini hasa kilikuwa chanzo cha kifo chake. Sonso alikuwa kijana na mwanamichezo tangu utoto wake. Sikuwahi pia kusikia akiumwa au kupata ajali. Nikaanza kusaili kujua nini hasa kimetokea.

Maneno ya Ruvu Shooting

Kwenye mazungumzo na baadhi ya vyombo vya habari na nyumbani kwa familia ya Sonso wakati wa maziko, Msemaji wa Ruvu Shooting – timu ambayo Sonso alikuwa akichezea kabla ya kufariki dunia, Masau Bwire, alitoa taarifa fupi kuhusu nini hasa kimetokea. Hii naichukulia ni taarifa rasmi zaidi kwa sasa.

Bwire alieleza Sonso alianza kuugua wakati wanajiandaa na mechi dhidi ya Simba Oktoba mwaka jana. Akaeleza kuhusu maumivu ya kwenye mguu, kuvimba kwa miguu na baadaye kuwa na malengemalenge na kupasuka. Akaeleza pia namna timu yake ilivyojitahidi kumtibia kwa kumpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na namna mchezaji na familia yake walivyokataa kutibiwa hospitalini hapo.

Halafu akasema wakaja kupata taarifa za kuzidiwa kwake na kifo chake wiki iliyopita. Kati ya kumpeleka mchezaji Muhimbili na taarifa za kifo chake ni takribani miezi mitatu na ushee ilikuwa imepita.

Kwa hiyo, tuseme Sonso ameugua kwa muda wa miezi mitatu kuanzia mara ya kwanza kulalamika maumivu mpaka kifo chake.

Kocha wake, Charles Boniface Mkwasa, naye alihojiwa na chombo kimoja cha habari na kusema anadhani sababu ya kifo cha Sonso ni upungufu wa damu kwa sababu alikuwa akivuja damu kutoka mguuni kwake.

Hiyo ndiyo taarifa pekee rasmi kutoka kwa waajiri wake iliyoeleza kidogo kuhusu kilichosababisha kifo cha mchezaji huyo.

Nimetazama pia mahojiano kati ya baba mzazi wa Sonso na waandishi wa habari. Mzee Mtoni kazungumza moja kwa moja, wao waliamua kufuata “njia mbadala” ya kumtibia mchezaji kutokana na maelezo aliyowapa hospitalini asingeweza kupata tiba hasa ya tatizo alilokuwa nalo. Maelezo ya baba mzazi wa marehemu ni Sonzo aliambiwa na wenzake kama atakubali kuchomwa sindano – ambayo ni sehemu ya matibabu ya hospitali, huo ndiyo ungekuwa mwisho wake wa kucheza mpira.

Bahati mbaya, Sonso hakukubali kuchoma sindano na mwisho umekuwa si wa kucheza mpira tu lakini ameondoka duniani moja kwa moja. Hili ndilo jambo ambalo sasa linafungua sehemu ya pili ya hoja yangu kwenye makala haya.

Sonso aliumwa nini hasa?

Kimaadili, ugonjwa wa mgonjwa huwa ni siri yake na daktari au mganga wake. Ugonjwa unaweza tu kuwekwa hadharani kwa namna mbili; mosi kama mgonjwa mwenyewe amekubali au familia yake imeridhia. Kwa sababu hatumfahamu mtu aliyekuwa anamtibia marehemu wakati wa uhai wake, tuseme ugonjwa uliomuondoa ndiyo huo wa miguu ulioelezwa na Bwire na baba mzazi wa Sonso.

Labda niseme vitu viwili kwanza. Mimi katika ngazi ya kidato cha tano na sita nilisoma masomo ya sayansi kwa mchepuo wa Fizikia, Kemia na Baiolojia. Wanafunzi wengi niliosoma nao sasa ni madaktari waandamizi katika hospitali tofauti Tanzania. La pili ni kwa sababu nimewahi kufanya kazi katika sekta ya michezo, ninafahamiana pia na baadhi ya madaktari wanaofanya kazi na waliowahi kufanya kazi katika vilabu vya mpira hapa nchini.

Sehemu kubwa ya makala imejengwa katika msingi wa mazungumzo yangu na wataalamu, kusaka maarifa kwenye mtandao na kidogo ninachojua kupitia elimu yangu na kufanya kazi kwenye tasnia ya soka.

Katika mazungumzo yangu na wataalamu wa afya ambao wameomba nihifadhi majina yao, kuna ugonjwa mmoja ambao umekuwa ukijirudia kuhusu maradhi yaliyomsumbua Sonso.

Kuna tatizo linajulikana kwa kitaalamu kwa jina la Deep Vein Thrombosis (DVT). Hilo ni tatizo la kiafya linalosababishwa na kuganda kwa damu kwenye mishipa ya damu. Ni kama vile damu inakuwa kwenye mabonge na wakati mwingine linakuwa bonge la mafuta.

Ukiingia kwenye Google hata sasa, utaona hili ni tatizo linaloweza kumkumba binadamu wa jinsia yeyote na umri wowote. Na mtandao unasema athari zake – endapo matibabu yatacheleweshwa, inaweza kuwa ni ulemavu wa kudumu na wakati mwingine kifo.

Dalili zikoje? Madaktari wanasema kwanza yanaanza kama maumivu kwenye mkono au mguu, baadaye kuvimba kwa mguu, baadaye mguu kuwa na vitu kama malengemalenge na rangi kubadilika kwenye eneo hilo na kisha eneo linaweza kupasuka na kuvuja damu. Kwa maelezo niliyoyasikia kuanzia kwa kina Bwire na kocha Mkwasa, nimezidi kushawishika inawezekana kabisa Sonso alikuwa na tatizo la DVT.

SOMA NA HII  UKWELI MCHUNGU....WACHEZAJI WENGI SIMBA NI WAZEE..HAWAWEZI KUBEBA UBINGWA WA AFRIKA...

Mtandaoni wanasema kujizuia na tatizo hilo, unaweza kujizuia kwa kutokaa chini kwa muda mrefu hasa ukiwa safarini au ukiwa umekaa tu kwenye kiti. Zipo pia dawa za kunywa za kuzuia kuganda kwa damu hata kama huna tatizo la aina yoyote.

Lengo la maelezo haya ni kuzuia mtu asijiweke kwenye hatari ya kuumwa. Kwamba hata wakati unaposafiri, hakikisha kila baada ya walau saa moja, uwe unasimama kidogo na kuchezesha miguu na mikono.

Nikawauliza madaktari, hiyo DVT ina dawa? Nikaambiwa kuna dawa za aina mbili. Ya kwanza ni kunywa vidonge au kuchoma sindano za kuyeyusha hilo donge la damu au mafuta linalozuia damu isitembee kama kawaida mwilini na njia ya pili ni kufanyiwa upasuaji wa kuondoa bonge hilo. Nimeambiwa – kwa uhakika kabisa, tiba zote hizo zinapatikana Tanzania.

Maswali ya kujiuliza

Kwenye tamaduni zenu, tuna msemo kazi ya Mungu haina makosa. Kwenye mazungumzo na wanahabari, Mzee Mtoni alisema kifo cha Sonso ni mapenzi ya Mungu na ilipangwa aondoke duniani – kama itakavyokuwa kwetu sote, kwa namna hiyo.

Ninaelewa maelezo hayo ya baba wa marehemu na kwa nini alisema hayo. Lakini kwa sababu sisi si mbuzi wala ng’ombe na Mwenyezi Mungu ametuumba pia kuwa viumbe vya kuwaza na kutafakari, ningependa kuuliza maswali kadhaa kupitia makala haya.

……Shooting ni daktari kamili wa magonjwa ya wanadamu? Kama daktari ni wa kiwango hicho, ilikuwaje hakuweza kuona mapema tatizo na kulibaini ilhali madaktari ambao nimezungumza nao kwa dakika tano tu kwa simu wameweza kuniambia kinagaubaga nini hasa linaweza kuwa tatizo lililomkumba Sonso.

Swali kubwa zaidi katika eneo hili ni moja; kwamba je ni vilabu vingapi vya Tanzania vina madaktari kamili wa binadamu walioajiriwa kufanya kazi kwenye timu za Ligi Kuu?

……Ruvu kusafiri na mchezaji ambaye miguu yake ilianza kuvimba na kuuma kwa kutumia usafiri wa barabara kurudi naye Pwani wakati kukaa chini kwa muda mrefu ni sehemu ya mambo yasiyotakiwa kwa wagonjwa wa miguu iliyovimba na kuuma? Kwa nini Sonso hakutafutiwa usafiri wa haraka kama vile ndege kurejeshwa Dar na kupelekwa kwa vipimo vikubwa?

…Ruvu Shooting– timu ya jeshi, ilikubali mchezaji atoe maelezo ya namna anavyotaka kutibiwa? Sonso alikuwa na mkataba wa kuitumikia timu hiyo na kwa hivyo klabu ilikuwa inawajibika kwa matibabu yake. Ilikuwaje Ruvu ikakubali mchezaji awaambie anataka kutibiwa namna gani.

Kuna uwezekano wa Cristiano Ronaldo leo kuumwa Manchester United na kuwaambia hataki hospitali na timu imwache akajihudumie mwenyewe na kukubaliwa? Ninachofahamu mimi ni timu zinaweza kumruhusu mchezaji kutibiwa mahali pengine endapo tu itafahamika huko anakokwenda kuna vifaa au utaalamu mkubwa zaidi wa kisayansi kuliko ule wanaoweza kuutoa wao. Lakini ni lazima klabu ndiyo ihusike na kumpeleka huko.

Katika umri wangu, nimejifunza sehemu ya mwisho ambayo mtu ana uwezo wa kufanya atakavyo au kufuata utaratibu binafsi ni kwenye taasisi za kidola kama jeshi.

Kwenye jeshi nafahamu unafuata utaratibu na protokali iliyopo na wakati mwingine huwezi hata kuuliza swali. Ilikuwaje mchezaji wa taasisi inayomilikiwa na jeshi akatoa masharti au maamuzi na taasisi ikamfuata na kumsikiliza badala ya yenyewe kusema “hapa sisi huwa tunaenda hivi?”.

…..wa Sonso akakaa kimya kati ya Novemba hadi Februari kufuatilia kuhusu afya ya mwajiriwa wao hadi kuishia kupewa taarifa siku ambayo hatimaye mchezaji alifariki dunia?

Hoja yangu ni, kama mchezaji aliondoka Oktoba, mkakaa hadi Novemba na hakuna dalili za kupona, si angalau kuna mtu angeamua kusema tunamchukua mchezaji kuanzia hapa na kuendelea? Nani huwa anafanya kazi za ustawi wa wachezaji (welfare) kwenye vilabu vyetu?

Nani hasa anashughulika na kuangalia maisha na maendeleo ya wachezaji wetu kiafya na kisaikolojia?

Ninafahamu kwamba jamii yetu ina imani za kishirikina kuanzia maofisini, shuleni, viwanjani na shambani. Ni rahisi sana kwa imani hizi kuingia kwa watu ambao pengine hawana maarifa makubwa zaidi ya kielimu kama walivyo wengi wa wachezaji na wazazi wetu.

…jukumu la kuzungumza na Sonso kama mtaalamu na kumpa mbadala?

Kwamba, pengine Sonso alihitaji mtu wa kumwambia anachoumwa ni DVT. Kama akichomwa sindano na ukawa mwisho wake wa mpira, Ruvu ingemtafutia shughuli nyingine ya kufanya ili maisha yake yaendelee. Mpira una shughuli nyingi. Lakini angalau angekuwa hai na kupata fursa ya kufurahi uhai wake na kusaidia waliokuwa wanamtegemea.

Angeambiwa pia mbadala wa huduma ya hospitali ni kuugua zaidi na kufa. Ukisoma taarifa za DVT mtandaoni, mgonjwa huwa na maumivu makali sana kiasi mwishowe kifo huwa ni sehemu ya kumpunguzia maumivu. Ni wazi Sonso alipitia katika maumivu ambayo hakuna anayesoma makala haya anaweza hata kufikiri. Ni maumivu ambayo mwili wako wenyewe unaona bora upoteze uhai kuliko kuendelea kuwa nayo.

Mtu huyo wa kuzungumza na Sonso angemwambia kama asingetibiwa hospitali, angekufa kwa maumivu makali na hiyo maana yake ni kwamba asingekuwa na msaada wowote kwa wanaomtegemea na asingekuwa walau na fursa ya kutazama mpira akiwa amepona. Angeambiwa pia kwa matibabu ya hospitali kulikuwa na nafasi ya kupona na kuendelea kucheza pia.

Makala haya yameandikwa na Ezekiel Kamwaga, na kuchapishwa kwanza kwenye wavuti la Mwanaspoti