Home news KUELEKEA MECHI DHIDI YA WAIVORY…MASTAA SIMBA WAVUNJA UKIMYA…WAELEZA JINSI WALIVYOKASIRISHWA…

KUELEKEA MECHI DHIDI YA WAIVORY…MASTAA SIMBA WAVUNJA UKIMYA…WAELEZA JINSI WALIVYOKASIRISHWA…


WACHEZAJI wa Simba wamewatoa hofu mashabiki na wakaapizana kwamba kwenye mechi za Shirikisho kuanzia Jumapili hii dhidi ya Asec Mimosas jijini Dar es Salaam hakuna kufanya kosa.

Simba wako kundi D na timu za RS Berkane ya Morocco, USGN ya Niger na Asec ya Ivory Coast.

Mastaa wawili wa Simba, Henock Inonga na Rally Bwalya wamesema kwamba wao kama wachezaji wamejipanga na wanataka kulipizia kile ambacho hawakukifanya kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa walipotolewa.

Bwalya ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuanza Jumapili kama kiungo mkabaji anasema; “Unajua suala la kuondolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu wachezaji wote tulikuwa na hasira na kuambiana huku kwenye Shirikisho ndio tunatakiwa kuonyesha ukubwa wetu kwa kupata ushindi mfululizo.”

Inonga ameahidi kuonyesha ubora wake kwa kupambana mwanzo mwisho. ”Kufanya vizuri kwangu maana yake nitaifanya timu kupata matokeo mazuri katika mashindano haya, tutawazuia wote na Simba kupata ushindi,” alisema.

“Malengo ya Simba ni kufanya vizuri katika mashindano haya na kufika mbali kwa maana hiyo kila mchezaji atapambana na kujituma kutimiza majukumu yake ili kuyafikia hayo tuliyokubaliana,” alisema.

Kati ya maandalizi ya Simba kuukabili mchezo huo ni mazoezi makali ambayo kocha wa Simba, Pablo Franco amebadili ratiba na kuweka awamu mbili kwa siku asubuhi yale ya Gym na jioni uwanjani.

Pia juzi benchi la ufundi lilikutana zaidi ya saa moja na kufanya uchambuzi wa kutosha kwa baadhi ya mechi walizocheza Asec Mimosas katika Ligi Kuu ya nchini kwao pamoja na mashindano ya kimataifa msimu huu.

Pablo, wasaidizi wake na mtaalamu wa uchambuzi wa video za wapinzani wa Simba, Culvin Mavunga waligundua wanakwenda kucheza na timu imara ndio maana katika ligi ya kwao inaongoza ikiwa imecheza mechi saba, imeshinda zote, imekusanya pointi 21, imefunga mabao 13 na imefungwa matatu.

Jambo jingine walilogundua na wameanza kulifanyia kazi haraka ni safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ina wachezaji hatari na wenye uwezo wa kufunga kama Karim Konate aliyeanza katika michezo yote. Michezo saba waliocheza Mimosas wamefunga mabao 13.

SOMA NA HII  KUHUSU ULE MPANGO WA YANGA KUJITANGAZI UBINGWA...DODOMA JIJI WAIKATALIA YANGA....