Home news KUHUSU UWEZO WA CHIKO USHINDI…NABI AKUNA KICHWA WEE..KISHA AKATOA OMBI HILI JIPYA...

KUHUSU UWEZO WA CHIKO USHINDI…NABI AKUNA KICHWA WEE..KISHA AKATOA OMBI HILI JIPYA YANGA…


KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi amewaambia mashabiki wa Yanga kwamba anahitaji siku 30 za mechi na mazoezi kuwaonyesha ubora uliomshawishi amsajili winga mpya, Chico Ushindi. 

Kocha Nabi alisema hajabahatisha kumsajili Ushindi, mchezaji mwenye hadhi ya kuvaa uzi wa Yanga ambaye walijiridhisha juu ya ubora wake wakiwa pia wanamjua kwa muda mrefu achilia mbali video za ubora wake ambazo mashabiki wanatambia mitandaoni.

Alisema kiufundi, Ushindi anahitaji siku 30 kuingia kwenye soka la ubora wa Yanga inayosaka kwa udi na uvumba ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho.

“Unajua hapa mwishoni hakuwa anatumika pale Mazembe lakini huyu ni mchezaji ambaye tunamjua kwa muda na tunajua ana ubora ambao utaisaidia timu yetu,” alisema Nabi ambaye ana uraia pacha wa Tunisia na Ubelgiji.

“Tumeona ni mtu sahihi kwa kikosi chetu, tunachofanya sasa kwanza ni kupandisha ufiti wa mwili wake, lakini pia tunataka ajue falsafa ya soka letu kwanza ili awe sambamba na wenzake, hili litahitaji kama siku 30,” alisema kocha huyo ambaye ufanisi wa timu yake umewapagawisha viongozi na mashabiki haswa wakiangalia mwenendo wa kuchechemea wa mtani wao wa jadi, Simba.

“Ila ndani ya muda huo tutakuwa tunampa dakika za kucheza taratibu kama dakika 20, 15 au hata 30 ili azoee taratibu na tunaamini ndani ya muda huo mashabiki watajua ubora wake,” aliongeza kocha huyo anayesaidiana na Cedrick Kaze kwenye benchi.

Katika kipindi hicho cha siku 30 alizopewa raia huyo wa DR Congo, Yanga itacheza mechi tano ambapo mbili ni za Kombe la Shirikisho la Azam na tatu za Ligi Kuu.

Mechi za Kombe la Shirikisho la Azam ni dhidi ya Mbao, Jumamosi leo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza na nyingine ya 16 Bora kwa ajili ya kuwania kutinga robo fainali ya michuano hiyo ambayo bingwa atacheza Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Mechi za Ligi Kuu ni dhidi ya timu za Mbeya City na Kagera Sugar nyumbani na ugenini dhidi ya Mtibwa kumalizia mzunguko wa kwanza.

SOMA NA HII  KWA TAKWIMU CHAMA AKASOME KWA SAIDO NTIBAZONKIZA...KAFUNIKWA VIBAYA MNOO...

Nabi alisema Ushindi mara atakapokuwa tayari ataongeza makali katika safu yao ya ushambuliaji kutokana na ubora wake wa kupiga krosi na hata kufunga.

Alisema staa huyo atakuwa ni mtaji mkubwa kwa washambuliaji wa kati kutokana na pasi zake za mabao ambazo ameshaanza kuzionyesha hata katika mazoezi ya timu hiyo inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa tofauti ya pointi 10 kileleni baada ya mechi 13.

“Ukimuona mazoezini utashuhudia hili ninalokwambia, anajua sana kutengeneza pasi za mabao. ni suala la muda watu watakuja kufurahia usajili huu muda mchache ujao,” alisema Nabi ambaye Yanga yake imeshinda mechi 11 na kutoa sare mbili tu kwenye Ligi dhidi ya Simba na Namungo.

“Tuna mechi nyingi bado ambazo atacheza na kuthibitisha ubora wake, lakini taratibu tutakuwa tukimpa muda tutakapoona anaimarika,” aliongeza kocha huyo ambaye mkataba wake na Yanga upo chini ya miezi sita kwa sasa.

Mechi ndani ya siku 30

Ndani ya siku 30 Yanga itakuwa na mechi tano, zikiwamo mbili za Kombe la ASFC na tatu za Ligi Kuu Bara.

Kesho Jumapili, Ushindi ataanza siku hizo 30 katika mechi ya hatua ya 32 Bora ya Kombe la ASFC dhidi ya Mbao jijini Mwanza na kama timu itapenya 16 Bora basi atakuwa na kazi nyingine kati ya Februari 7-12 kucheza na mshindi kati ya Biashara United na Mbeya Kwanza.

Katika ligi atawavaa Mbeya City Feb 5, kisha Manungu kucheza na Mtibwa Sugar Februari 23 na Februari 27 watamalizana na Kagera Sugar.