Home Makala KWA VYOVYOTE VILE….MATANO KUMNG’OA MORRISON SIMBA…CHAMA ATAJWA…

KWA VYOVYOTE VILE….MATANO KUMNG’OA MORRISON SIMBA…CHAMA ATAJWA…


KIWANGO cha Simba msimu huu sio cha kuridhisha kwenye Ligi Kuu Bara kutokana na aina ya matokeo wanayopata pamoja na kile wanachoonyesha wachezaji wa kikosi hicho katika kila mechi.

Kuna baadhi ya wachezaji walitegemewa kufanya makubwa mwanzoni mwa msimu huu kama Bernard Morrison aliyeshindwa kufanya hivyo kutokana na kile anachokionyesha Msimbazi.

Kwenye msimu huu, Morrison mechi aliyocheza katika kiwango cha juu ni ile ya mzunguko wa kwanza hatua ya mtoano Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows ya Zambia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Ukiachana na mechi hiyo, Morrison amekuwa mchezaji wa kawaida ndani ya Simba na hata kukosa baadhi ya mechi muhimu na sio kwa bahati mbaya, bali kiwango chake hakiriridhishi benchi la ufundi.

Uongozi wa Simba haujaweka wazi kinachoondelea kati yao, ukiachana na sakata lake la kusimamishwa, lakini Morrison ila kuna mambo ambayo amekuwa akifanya yanayoweza kumuondoa katika kikosi hicho mwisho wa msimu huu baada ya mkataba wake kumalizika.

Makala haya inakuletea mambo yanayoweza kumuondoa Morrison Simba mwisho wa msimu licha ya kusajiliwa kwa mbwembwe nyingi na miamba hiyo ya soka nchini akitokea Yanga misimu miwili iliyopita.

KIWANGO

Katika kipindi cha miaka miwili Morrison aliyopo Simba kuna baadhi ya mechi amekuwa akicheza katika kiwango bora na kuacha gumzo kwa wengi kutokana na uwezo alionao.

Jambo la kutofurahishwa kwa mabosi na hata wanachama ni baada ya kuonyesha kiwango bora katika mechi flani flani zilizopita na kisha kuchukua tena muda mrefu kucheza kwa ubora mpaka wakati mwingine kuwa mchezaji wa kutokea benchi.

Katika mizunguko 14 ya Ligi Kuu, Morrison hakuna hata mechi moja aliyocheza katika kiwango ambacho kinatamanisha muda wote, bali amekuwa mchezaji wa kawaida.

Kutokana na Simba kuwekeza pesa nyingi kwake katika usajili walioufanya na kile ambacho amekuwa akikionyesha mpaka sasa viongozi hawajafanya mazungumzo naye kumuongezea mkataba mpya licha ya kuwa unaelekea ukingoni.

NIDHAMU

Jambo lingine linaloweza kumuondoa katika kikosi ni matukio mengi ya utovu wa nidhamu anayofanya kwa nyakati tofauti ndani ya kikosi hicho.

Awali, uongozi wa Simba uliamua tu kuchagua kukaa kimya, kwani Morrison amekuwa na mikasa mingi ya utovu wa nidhamu anayoyafanya ndani ya kambi na sehemu nyingine.

Inadaiwa kwama viongozi wa Simba wamekuwa wakichukizwa na masuala hayo. Kuna yale matukio ya wazi ya utovu wa nidhamu kama alilofanya mjini Kigoma katika mechi ya fainali Kombe la Shirikisho (ASFC) msimu uliopita dhidi ya Yanga na kuigharimu timu kwa kukosa mechi tatu muhimu ikiwemo ile na Ngao ya Jamii msimu huu.

SOMA NA HII  BAADA YA KUTAKATA KWENYE LIGI YA MOROCCO...MSUVA HUYOOO ULAYA...AITAJA LA LIGA YA HISPANIA...

UREJEO WA CHAMA

Wakati Luis Miquissone anasajiliwa na Al Ahly ya Misri na Clatous Chama kwenda zake RS Berkane ya Morocco miongoni mwa wachezaji waliopewa nafasi kubwa na hata kutegemewa kuziba nafasi za nyota hao ni Morrison.

Matumaini ya mashabiki yalikuwa makubwa kwake na waliamini anakwenda kuwa nyota wa kikosi kwa kuonyesha kiwango bora msimu huu na jina lake kuimbwa zaidi ya msimu uliopita.

Mambo yamekuwa tofauti kwa Morrison ambaye sasa ni mchezaji wa kawaida na sio tegemeo katika kikosi cha kwanza, ndio maana Simba inacheza bila uwepo wake na hakuna hata anayesumbuka kujiuliza juu yake.

Kushindwa kuonyesha makali kwa mchezaji huyo kumewafanya mabosi wa Simba kutumia nguvu nyingi kumrudisha Chama kikosini ambaye kama ataendelea kuwa katika ubora wa kabla ya kuondoka nafasi ya Morrison kubaki itakuwa finyu.

NJE YA UWANJA

Viongozi wa Simba wakati wanafanya usajili wa Morrison kutoka Yanga mbali ya kiasi kikubwa cha fedha walichotumia miongoni mwa mambo waliyoyaweka wazi ni kuwa nyota huyo atakuwa bora zaidi uwanjani kuliko nje.

Ndani ya misimu miwili mambo yamekuwa tofauti kwa nyota huyo kwani amekuwa na mambo mengi nje ya uwanja yasiyokuwa ya lazima kama yale ya ndani ya uwanja anayotakiwa kuyafanya.

Morrison ana vituko vingi anavyofanya nje ya uwanja kama vile kubaki na nguo ya ndani kisha kutupia picha katika mitandao ya kijamii jambo ambalo kwa desturi za Kitanzania sio la kupendeza.

Nguvu anayotumia nje ya uwanja kufanya mambo ambayo sio ya lazima angewekeza ndani ya uwanja pengine angekuwa na kiwango bora zaidi ya sasa.

WACHEZAJI WA KIGENI

Kabla ya kuanza msimu ujao Simba wataingia sokoni kutafuta nyota wapya wa kigeni si chini ya watatu ili kuja kuongeza makali kikosini kwa ajili ya msimu ujao.

Katika kikosi cha sasa kuna wachezaji 12 wa kigeni kama kanuni za Ligi Kuu Bara zinavyotaka na ili kuingiza wengine wapya maana yake ni lazima waachane na baadhi ya waliopo sasa.

Hata hivyo, hili litatokana na kuendelea na kanuni zilizopo za uendeshaji wa ligi, vinginevyo zikibadilishwa itategemea na mabadiliko hayo.

Makala haya yaliandikwa na Thobias Sebastian, na kuchapiswa kwanza kwenye wavuti la Mwanaspoti