Home news PAMOJA NA YANGA KUCHOONGA SANA SAFARI HII..SIMBA WAIHENYESHA KWA MIAKA 10…ISHU IKO...

PAMOJA NA YANGA KUCHOONGA SANA SAFARI HII..SIMBA WAIHENYESHA KWA MIAKA 10…ISHU IKO HIVI…


PALIPO Simba na Yanga, pana uhondo, raha, karaha, ushindani, vituko na rekodi zinazosisimua, zinazowafanya mashabiki wao, kutamba kila kona.

Ni klabu zilizo na nguvu, na kutokana na utajiri wa mashabiki zilionao, zimejitofautisha na timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, hilo linadhihirishwa na rekodi zao.

Zinaongoza kwa kunyakua mataji mengi ya Ligi Kuu Bara, Yanga inamiliki mataji 27 na Simba 22, jambo linalodhihirisha nguvu yao nchini.

Ukiachana na rekodi hizo, Mwanaspoti linakuchambulia ndani ya miaka 10 ambayo Simba ilitwaa ubingwa mara tano, Yanga (4) na Azam (1), nani kachukua ubingwa kwa pointi nyingi zaidi, wakipokezana kwa nyakati tofauti.

2021: SIMBA POINTI 83

Simba ilinyakua taji la Ligi Kuu (2021), ikikusanya pointi 83. Katika mechi 34, ilishinda 26, sare tano, kupoteza mechi tatu na ilifunga mabao 78 huku ikiruhusu mabao 14.

Wakati Simba inatamba na ubingwa, mtani wake wa jadi Yanga alimaliza nafasi ya pili kwa pointi 74, akiwa na mabao ya kufunga 52 na ya kufungwa 21.

2020: SIMBA POINTI 88

Simba ilijikusanyia pointi 88, wakati inanyakua ubingwa (2020), ambapo katika mechi 38, ilishinda 27, sare saba na ilifungwa nne na ilikuwa mabao ya kufunga 78 na kufungwa 21.

Yanga ilishika nafasi ya pili, ikimaliza na pointi 72 na ilikuwa na mabao ya kufunga 45 na kufungwa 28.

2019: SIMBA POINTI 93

Simba ilitangazwa bingwa (2019) baada ya kumaliza na pointi 93, katika mechi 38, ilishinda 29, sare sita na ilifungwa tatu na ilimaliza na mabao ya kufunga 77 na kufungwa 15.

Ni mwaka ambao Yanga ilimaliza nafasi ya pili kwa pointi 86 na mabao ya kufunga 56 na kufungwa 27.

2018: SIMBA, POINTI 69

Mwaka 2018 Simba ilipoza machungu kwa kuchukua ubingwa kwa pointi 69 baada ya kulikosa taji hilo kwa muda mrefu, katika mechi 30, ilishinda 20, sare tisa na ilifungwa mmoja, ilimaliza na mabao ya kufunga 62 na kufungwa 15.

Azam FC ilimaliza nafasi ya pili kwa pointi 58 na ilikuwa mabao ya kufunga 35 na kufungwa 16.

2017: YANGA POINTI 68

Yanga ilitangazwa bingwa (2017), ikimaliza na pointi 68 katika mechi 30, ilishinda 21, sare tano na ilifungwa nne na ilifunga mabao 57 na kufungwa mabao 14.

Simba ilimaliza nafasi ya pili mwaka huo, ilivuna pointi 68 kwa tofauti ya mabao 50 kwa 17 na mtani wake wa jadi Yanga.

2016: YANGA POINTI 73

Yanga ilichukua ubingwa (2016) ikimaliza na pointi 73 katika mechi 30 ilishinda 22, sare 7 na ilifungwa moja na ilimaliza na mabao 70 na kufungwa 20.

Azam FC ndio ilimaliza nafasi ya pili kwa pointi 64 na ilimaliza na mabao 47 na kufungwa 24.

SOMA NA HII  INONGA ARUDISHA MKWANJA WA YANGA...AMKIMBIA MAYELE AIRPORT...SIMBA WAPEWA MCHONGO CAF...

2015: YANGA POINTI 55

Yanga ilitangazwa mabingwa (2015) ikiwa na pointi 55 zilizopatikana baada ya kucheza mechi 26, ilishinda 17, sare nne na ilifungwa tano na ikafunga mabao 52 na kufungwa 18.

Mshindi wa pili ilikuwa Azam FC ilimaliza na pointi 49 na mabao 36 na kufungwa 18.

2014: AZAM FC POINTI 62

Azam FC ilibadilisha upepo wa Jangwani na Msimbazi, baada ya kunyakua ubingwa (2014) kwa pointi 62 ambapo katika mechi 26, ilishinda 18 na sare nane, huku ikiwa na mabao ya kufunga 51 na ya kufungwa 15.

Yanga kwa mwaka huo ilimaliza nafasi ya pili kwa pointi 62 na kufunga mabao 61 na ya kufungwa 19.

2013: YANGA POINTI 60

Yanga mwaka 2013 ilinyakua taji la Ligi Kuu kwa pointi 60 katika mechi 26, ilishinda 18, sare sita na ilifungwa miwili na ilikuwa na mabao 47 na kufungwa 14.

Azam FC ilimaliza nafasi ya pili kwa pointi 54 na jumla ya mabao 46 na kufungwa 20.

2012: SIMBA POINTI 62

Mwaka 2012 Simba ilichukua ubingwa kwa pointi 62 katika mechi 26, ilishinda 19 na sare tano na ilifungwa michezo miwili, huku ikimaliza na mabao 47 na kufungwa 12.

Azam FC ilimaliza nafasi ya pili kwa pointi 56 na mabao 40 na ya kufungwa 15.

Ndani ya miaka 10 Simba imewahi kuchukua ubingwa kwa pointi za juu zaidi 93 mwaka 2019 rekodi ambayo haijafikiwa na Yanga.

Yanga ndani ya miaka 10 pointi zake za juu zaidi ni 73 mwaka 2016.

Katika kipindi cha miaka 10, Simba ndio timu inayoongoza kuchukua ubingwa mara nyingi, ikichukua mara tano, Yanga mara nne huku kwa upande wa matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC ikichukua mara moja tu.

Simba imefunga jumla ya mabao 342, ikifungwa 77, wakati Yanga ikifunga mabao 226, ikitikiswa nyavu zake mara 93, huku Azam ikifunga mabao 51 ikiruhusu kufungwa mabao 15.

Straika wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua anasema klabu hizo zinazidiana rekodi, anachokiona cha muhimu ni ubingwa.

“Ni timu zenye rekodi za kuvutia ambazo zipo tofauti, Simba inaongoza ndani ya miaka hiyo kuwa na pointi nyingi, lakini Yanga inaongoza kwa kuchukua mataji mengi 27, kiukweli ni timu ambazo haziishiwi raha,” anasema.

Kiungo wa zamani wa Simba, Shaban Kisiga anasema timu hizo zinashindana maeneo tofauti, jambo aliloliona linanogesha Ligi Kuu na kutoa burudani kwa mashabiki wao.

“Ndani ya miaka hiyo Simba inaonekana kuchukua taji kwa kumaliza na pointi nyingi, Yanga nayo inamiliki mataji mengi, hizo ni klabu zenye ushindani mkali sana,” anasema.