ACHANA na matokeo ya jana, unaambiwa ndani ya kikosi cha Yanga kinara wa mabao ni Fiston Mayele aliyetupia tisa katika Ligi Kuu, akiwa ameiteka asilimia kubwa ya nchi kwa staili yake ya kushangilia, eti kocha wake Nesreddine Nabi ametoa tathmini ya kazi yake akisema ni asilimia 60 tu.
Kocha Nabi alisema mpaka sasa Mayele amefanya kazi yake kwa asilimia 60 tu, licha ya mashabiki kuzidi kupagawa na mabao yake na staili yake ya kushangili kwa kupiga mkono na kutetema.
Nabi alisema bado Mayele anaweza kufikia asilimia 40 ya kazi yake, lakini kuna vitu ambavyo ataendelea kuboreshwa taratibu.
“Mimi ndio nimemleta Mayele nilipomuona nilijua kwamba ni mtu atakayefanya makubwa sio tu Yanga, bali kwa ligi kwa ujumla kwa vile nilikuwa hapa msimu uliopita na kuona ni aina gani ya mshambuliaji atakayefanya kazi bora hapa.
“Hadi sasa naweza kusema amefanya kazi kwa asilimia 60 tu, ingawa bado kuna nafasi ya kufikia hata asilimia 100 yapo mambo anayotakiwa kumboresha zaidi,” alisema Nabi na kuongeza;
“Jambo kubwa ni kujiweka katika mazingira ya kufunga zaidi mara nyingi anakuwa anapokea mpira akiwa anaangalia eneo letu.”
Nabi alisema Mayele sasa anatakiwa kuboreshwa kupokea mipira mingi akiwa anaangalia lango la wapinzani hapo atafunga kirahisi.
Aliongeza kwamba kitu kingine ambacho kimesalia ni viungo wa pembeni kuwa na ubora wa kumtengenezea mashambulizi mazuri kwa kuwa na krosi rafiki.
“Tuna changamoto ya viungo wanaocheza pembeni bado hawajajua ni aina gani ya mipira ya ya kumpa Mayele, angalia krosi aliyopiga Saido (Ntibazonkiza) wakati tunacheza na Mtibwa mipira kama ile ya chini na juu inatakiwa iwe mingi.”
Marefa na mabao kukataliwa
Aidha Nabi aliongeza, Mayele bado amekuwa akikumbana na changamoto mbili nje ya ufundi wa timu yao kwa kuchezewa vibaya na mabeki, pia mabao yake ya wazi yakikataliwa.
“Wachezaji wakubwa wanalindwa kila mtu anaigiza shangilia ya Mayele hata wapinzani wetu, lakini jina lake linafanya mabeki kumkamia ila waamuzi hawaoni hilo,” alisema Nabi na kuongeza;
“Wachezaji wakubwa Ulaya wanalindwa angalia Messi (Lionel) na hata Ronaldo (Cristiano) yapo mazingira ya kulindwa.
“Pia kuna mabao yake mazuri tu yanakataliwa kwa sasa angekuwa na mabao hata 11 ingempa nguvu zaidi za kukimbia kufunga zaidi.”