KUFUNGWA kunauma, ukitaka kuamini hilo ni namna mastaa wa Simba walivyotua kinyonge Uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, baada ya kutoka kufungwa na RS Berkane ya Morocco.
Kipigo cha mabao 2-0 ambacho Simba imekumbana nacho huko Morocco ni cha kwanza kwao kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hadi sasa Simba imecheza mechi tatu kwenye hatua hiyo na kuvuna pointi nne, baada ya kuifunga ASEC ya Ivory Coast kwa mabao 3-1 na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Gendarmerie huko Niger.
Baada ya kutua jana Jumanne, Machi Mosi, 2022 alianza kutoka kiungo Jonas Mkude akiwa amevaa barakoa na kofia iliyoziba uso, zilipita dakika takribani tano akatoka kipa Beno Kakolanya, zikapita dakika tano nyingine akafuata Erasto Nyoni.
Baada ya hapo wakatoka wachezaji wengine kwa pamoja, huku sura zao zikiwa hazina furaha, jambo ambalo baadhi ya mashabiki wao waliishia kuwashangaa.
Gazeti la Mwanaspoti iliwashuhudia baadhi ya mashabiki wakishangazwa na baadhi ya wachezaji ambao walificha sura zao wakati wanawasili uwanja wa ndege, jambo ambalo baadhi yao liliwanyima uhuru wa kuwafuata kupiga nao picha.
Ndipo mkuu wa kitengo chao cha Habari, Ahmed Ally aliposema hawana wasiwasi kupoteza mbele ya RS Berkane, kwasababu sifa ya kundi lao D kila timu imeshinda kwao.
“Kila timu imeshinda kwao, tunasubiri kushinda kwetu, safari ilikuwa ndefu tunashukuru tumefika salama, wachezaji wamechoka watapata muda wa kupumzika tayari kujiandaa dhidi ya Biashara United.” amesema.