KASI ya Fiston Mayele katika ufungaji mabao msimu huu imemuibua kocha mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ambaye ameweka wazi kuwa staa huyo amekuwa na wakati mgumu akikamiwa na wapinzani na kuomba mamlaka zinazohusika na usimamizi wa michezo kumlinda.
Tangu amejiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu, Mayele amekuwa wa moto ambapo kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Geita Gold, tayari alikuwa amehusika kwenye mabao 12 ya Yanga kwenye Ligi Kuu Bara pekee akifunga mabao tisa na kuasisti mara tatu.
Mayele juzi Jumapili aliiongoza safu ya ushambuliaji ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold, uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambapo Yanga waliibuka na ushindi wa goli moja bila.
“Ni kweli tunakubaliana na ukweli kwamba ligi ya msimu huu ina ushindani mkubwa na kila timu inapambana kuhakikisha inafanya vizuri na kupata pointi katika kila mchezo wanaocheza, lakini kuna wakati vita hizi za uwanjani zimekuwa zikisababisha majeraha yasiyo na ulazima kwa baadhi ya wachezaji muhimu.
“Kwa mfano kwetu mchezaji kama Mayele amekuwa akichungwa sana na walinzi wa wapinzani na kusababisha wakati mwingine awe katika wakati mgumu na hatari ya kupata majeraha ambayo yanaweza kuwa pigo kwetu”