Yanga imeendelea kuweka rekodi nyingine ya ubora ikitoa makipa bora wawili katika makipa ambao lango lao lipo salama.
Katika takwimu ambazo zimetoka Bodi ya Ligi Kuu zinaonyesha kipa wa Yanga Diara Djigui na Aishi Manula wa Simba kwasasa wako katika nafasi moja wakiwa na mechi 9 ambazo hawajaruhusu bao ‘clean sheets kwenye mechi 17 ambazo timu zote zimecheza mpaka sasa ligi ilipofikia.
Hata hivyo makipa hao wawili ambao ni chaguo la kwanza katika klabu zao wametofautiana katika idadi ya mabao waliyoruhusu ambapo Manula ameruhusu mabao 5 huku Diara akiruhusu mabao 4.
Nyuma ya makipa hao yupo kipa Aboutwalib Mshery ambaye ni kipa chaguo la pili katika kikosi cha Yanga ambaye ana mechi 8 bila kuruhusu bao.
Katika mechi hizo Mshery amefanikiwa kumaliza mechi tatu bila kuruhusu bao akiwa na jezi ya Yanga huku 5zilizobaki akihama nazo akitokea Mtibwa Sugar.
Kipa huyo kijana alisajiliwa na Yanga katika dirisha dogo la usajili msimu huu akitokea Mtibwa akija kusaidiana na Diara katika lango la vinara hao wa Ligi.
Nyuma ya makipa hao wapo makipa wa zamani wa Yanga Metacha Mnata ambaye sasa anaichezea Polisi Tanzania na Mussa Mbisa wa Coastal Union aliyewahi kuichezea Yanga ya vijana ambao wote wawili wana mechi 6 kila mmoja bila kuruhusu bao.