KIUNGO mshambuliaji tegemeo wa Yanga hivi sasa, Mrundi Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’ ameondolewa kwenye mipango ya kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi kwa muda wiki tatu kutokana na tatizo la goti.
Hiyo itamfanya akose mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC FC utakaochezwa Machi 19, mwaka huu kwenye Uwanja Mkapa, Dar.
Daktari wa Viungo wa Yanga, Youssef Ammar alisema kuwa kiungo huyo ataanza kuonekana uwanjani kucheza michezo ya ligi na Kombe la FA baada ya wiki tatu.
Ammar alisema kuwa kiungo huyo tayari alishaanza kupumzishwa kwa wiki moja akibakisha mbili huku akiendelea na matibabu.
Aliongeza kuwa hivi sasa kiungo huyo anafanya program maalum ya gym pekee kwa ajili ya kulinda fitinesi yake ili isipotee mara atakaporejea uwanjani kuipambania timu yake.
“Saido taarifa zake zinaripotiwa tofauti, ukweli ni kwamba baada ya vipimo kufanyika kutokana na majeraha yake, ikashauriwa apumzike kwa wiki tatu pekee na baada ya hapo atakuwa fiti tayari kurudi uwanjani.
“Tayari amemaliza wiki moja kati ya hizo alizopewa, hivi sasa amebakisha mbili ambazo zinamalizika na hadi kufikia wiki ijayo atakuwa amemaliza muda huo wa kukaa nje ya uwanja.
“Hivyo mchezo atakaoukosa ni ule wa ligi dhidi ya KMC pekee, lakini hiyo mingine inayofuatia atakuwa sehemu ya kikosi dhidi ya Azam FC,” alisema Ammar.