KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama hajarejea kwa bahati mbaya ndani ya kikosi hicho, data zinaonyesha katika mechi saba alizocheza za Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Azam (ASFC) kahusika na mabao 10.
Chama alirejea nchini Januari akitokea klabu ya RS Berkane ya Morocco, ambapo ujio wake uliwashitua wengi na kuona ameshuka kiwango kilichomfanya aitamani Ligi Kuu, hata hivyo staa huyo anazikanusha fikra hizo kwa vitendo.
Gazeti la Mwanaspoti linakuchambulia kwa njia ya data, matokeo ambayo Simba ilipata kabla ya Chama kurejea na baada ya staa huyo kujiunga nao kwa mara nyingine.
Simba bila ya Chama, katika mechi 12 ilijikusanyia pointi 24, mabao 14 na ilitoka suluhu tatu dhidi ya Biashara United, Coastal Union na Yanga.
Katika pointi 24, aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Didier Gomes aliyefutwa kazi Oktoba 26 alivuna nne na bao moja dhidi ya Biashara United (0-0) na Dodoma Jiji (1-0), chini ya Hitimana Thierry, zilipatikana pointi nne, bao moja dhidi ya Polisi Tanzania (1-0) na Coastal Union (0-0).
MECHI ZA CHAMA
Chama alikaa jukwaani Simba ikichapwa bao 1-0 na Mbeya City, aliingia kipindi cha pili ikitoka suluhu dhidi ya Mtibwa Sugar, alianza dhidi ya Kagera Sugar ikichapwa bao 1-0 na alicheza dhidi ya Prisons, ikishinda bao 1-0.
Chama alifunga dhidi ya Mbeya Kwanza, Simba ikishinda 1-0 na alifunga bao moja kwenye ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Biashara na alifunga bao moja Simba ilipoichapa Dodoma Jiji mabao 2-0.
Pointi ambazo Simba imevuna Chama akiwa ndani ni 13 ambazo zikijumuishwa na 24 za mechi ambazo hakuwepo inakuwa jumla ya pointi 37.
Mechi ambazo Simba ilicheza kabla ya Chama kurejea ni dhidi ya Biashara United (0-0 Karume), ilishinda dhidi ya Dodoma Jiji (1-0, Jamhuri Dodoma), ilishinda dhidi ya Polisi Tanzania (1-0, Mkapa) Coastal Union (0-0, Benjamin Mkapa), ilibwaga Namungo (1-0, Benjamin Mkapa), ikaichapa Ruvu Shooting (3-1, CCM Kirumba).
Michezo mingine Simba ilicheza dhidi ya Geita (2-1, Mkapa), dhidi ya Yanga (0-0, Mkapa), ilishinda dhidi ya KMC (4-1, Ali Hassan Mwinyi, Tabora) na ilishinda dhidi ya Azam FC (2-1, Mkapa).
MABAO 4, ASISTI 4 ASFC
Chama alifunga kwenye Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), dhidi ya Dar City Simba ikishinda 6-0, na pia akapiga hat-trick dhidi ya Ruvu Shooting dakika 25, 27 na 72 wakati Simba ikishinda 7-0. Alitoa jumla ya asisti nne katika mechi hizo mbili.