NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga, amesema anaamini kwamba ipo siku atawaanzisha washambuliaji wake wawili kwenye mechi za ushindani ambao ni Fiston Mayele na Heritier Makambo.
Nyota hao wawili raia wa DR Congo, kwenye mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu wakati Yanga ikishuka dimbani mara 17, hawajafanikiwa kucheza pamoja kutokana na mfumo wa mwalimu huyo ambaye anapenda kutumia mshambuliaji mmoja halisia.
Katika mechi zote 17, Mayele amekuwa chaguo la kwanza, huku Makambo akitokea benchi akipishana na Mkongomani mwenzake huyo.
Kwa sasa Mayele amekuwa akicheza sambamba na Saidi Ntibazonkiza kwenye eneo la ushambuliaji na kuonekana pacha yao imeanza kuiva.
Nabi alisema: “Unaona kwa sasa ni Mayele anaanza kikosi cha kwanza kwenye mechi zetu, lakini yupo na mshambuliaji mwingine Makambo, hawa wote ni washambambuliaji wazuri na wanatimiza majukumu yao.
“Ipo wazi kwamba kuna siku wote watacheza pamoja kulingana na mchezo utakavyokuwa, ni suala la kusubiri kwani ambacho tunahitaji kwenye mechi zetu zote ni ushindi na si kingine.”
Mchezo ujao kwenye Ligi Kuu Bara, Yanga itacheza dhidi ya KMC unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, Machi 19, mwaka huu.