KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi ambaye juzi alikuwa uwanjani kuishuhudia Simba ikifanya yake dhidi ya RS Berkane, amepanga kuja na mikakati mipya itakayompa matokeo mazuri ya ushindi ili kufanikisha malengo ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara akianza na KMC FC.
Yanga mchezo wake wa ligi unaofuatia ni dhidi ya KMC utakaopigwa Jumamosi hii saa moja kamili usiku kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo uliopita wa ligi uliozikutanisha timu hizo, ulimalizika kwa KMC kufungwa 2-0 ambao wao walikuwa wenyeji wa mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.
Nabi alisema kuwa wapinzani wasitarajie mbinu alizozitumia katika mzunguko wa kwanza, basi ndiyo atakazozitumia huku akiwataka kujipanga vema mara watakapokutana uwanjani.
Nabi alisema kuwa amepanga kuja kivingine katika michezo ijayo ya ligi, kutokana na kubadili mbinu na aina za uchezaji baada ya kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wake tegemeo waliokuwepo katika kikosi cha kwanza.
“Niwapongeze wachezaji wangu kwa kumaliza vizuri mzunguko wa kwanza bila ya kupoteza, malengo yangu ni kuona tukimaliza ligi bila ya kupoteza ili tuendelee kukaa kileleni hadi mwishoni mwa msimu.
“Katika mzunguko huu wa pili huenda tukaingia uwanjani kwa mbinu tofauti za mchezo, hiyo ni kutokana na baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kuwakosa ambao wana majeraha.
“Lakini yapo maingizo mapya ya wachezaji ambao wamepona watakuwepo sehemu ya wachezaji watakaoingia katika kikosi cha kwanza ambao ni Chico (Ushindi), Kibwana (Shomari), Bryson (David) na wengine waliokuwa hawapati nafasi Ambundo (Dickson), Nkane (Denis) na Sure Boy (Salum Aboubakary),”alisema Nabi.