Home Habari za michezo WAKATI SIMBA IKIZIDI KUVUNJA REKODI ZA AL AHLY CAF…BARBARA KUMBE ALISHALIONA HILO...

WAKATI SIMBA IKIZIDI KUVUNJA REKODI ZA AL AHLY CAF…BARBARA KUMBE ALISHALIONA HILO MAPEMA…


KIKOSI cha Simba mchana wa leo kimekula msosi nchini Benin kikijiandaa kuwavaa Asec Jumapili, huku mashabiki wa Mnyama wakiweka rekodi ya kutazamwa, kulinufaisha Shirikisho la Soka Afrika (CAF). 

Simba imekuwa ndio klabu inayotazamwa kwa wingi na mashabiki kupitia akaunti za mitandao ya kijamii za CAF, ikiwamo Youtube, kulinganisha na timu nyingine kongwe Afrika ikiwamo TP Mazembe ya DR Congo na Al Ahly ya Misri.

Mzuka wa Simba kimataifa umekuwa ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez aseme Simba inaongoza kwa kuingiza mashabiki katika mashindano ya Afrika kwa ngazi ya klabu kuliko timu yoyote kwa mujibu wa takwimu alizoonyeshwa na CAF.

Barbara alisema hayo siku chache kabla ya kuvaana na ASEC Mimosas katika mechi ya kwanza iliyopigwa mwezi uliopita na Simba kushinda mabao 3-1, huku mashabiki 35,000 wakiruhusiwa kulishuhudia Kwa Mkapa.

Achana na umati huo wa Uwanjani, lakini tathmini iliyofanywa kwenye akaunti za CAF mitandaoni imebaini kwamba mechi za Simba katika mashindano hayo zinaongoza kwa kutazamwa na watazamaji wengi kwenye ‘CAF TV’ ndani ya Youtube, ikifuatiwa na Al Ahly ya Misri ambayo ni tajiri kuliko Simba.

CAF, ilianza rasmi kutupia video fupi za matukio ya mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2020-2021 kuanzia hatua ya makundi hadi fainali.

Rekodi zinaonyesha pambano lililotazamwa zaidi ni lile la Simba vs Al Ahly la msimu uliopita ambapo Simba ilishinda 1-0, kwani lilitazamwa na mashabiki zaidi ya milioni moja, huku maoni yakiwa zaidi ya 800.

Mechi iliyoshika nafasi ya pili baada ya ile ya Simba na Al Ahly ni Simba na AS Vita iliyopigwa Dar ikitazamwa na mashabiki 597,000 na ile ya ugenini ambayo Simba ilishinda bao 1-0 ina watazamaji 529,000 katika chaneli ya CAF TV. Mechi ya Simba na El Merrikh ya Dar, Mnyama akishinda 3-0 ilitazamwa na watazamaji zaidi ya 393,000.

SOMA NA HII  MSEMAJI WA MTIBWA AWAPA 'MAKAVU LIVE' MANARA NA AHMED ALLY..." WANASHINDWA KUJITAMBUA"....

Mechi nyingine zilizotazamwa kwa wingi pia zikuhusisha Simba ni robo fainali dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini iliyopata watu 177,000 na ile ya Simba na Al Ahly iliyopigwa Cairo ikitazamwa na watu 169,000.

Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya msimu uliopita kati ya Al Ahly ya Misri na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini hadi sasa imetazamwa na watu 153,000 tu, kuonyesha namna gani Simba inavyotisha ndani ya CAF TV.

Msimu huu, Simba ikishiriki Shirikisho, pambano lao la kwanza na Asec la Dar ndiyo limetazamwa zaidi na watu 183,000, ikifuatiwa na Simba na RS Berkane uliopigwa kwa Mkapa ukitazamwa na watu 127,000. Ule wa ugenini baina ya timu hizo ulipata watazamaji 115,000.

Hata hivyo, Simba kuna mechi zake mbili za msimu uliopita zimepata watazamaji wachache ikiwamo mchezo wa ugenini dhidi ya El Merrikh ya Sudan uliopata watu 56,000 na ule wa USGN ya Niger uliopigwa ugenini msimu huu uliopata watu 97,000 hadi sasa. Tafsiri ya kutazamwa huko ni kwamba CAF TV na mitandao yao itajiongezea kipato zaidi siku zijazo kupitia ubora na mvuto wa Simba.

WASIKIE WADAU

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa, alisema; “Ni jambo zuri, inatengeneza fursa kwa wachezaji wa ndani na wa nje wanaokipiga ndani simba kuonekana na kufuatiliwa kwa ukaribu na hata hivyo naona pia kuna faida kubwa wanaipata CAF kupitia Simba.” Staa wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella alisema kuwa jambo hili linaonyesha ukubwa wa Simba kimataifa na linaweza kuwa chachu zaidi ya klabu hii kujitangaza kimataifa zaidi lakini kwa baadhi ya watu wanaweza kushangaa kuona hivi lakini kwangu lipo tofauti. “Hii ni kutokana na mvuto walionao Simba pamoja na matokeo mazuri.”

“Wachezaji wengi watavutika kutua msimbazi kwani kila mchezaji anapenda kuonekana ulimwenguni ili kujitengenezea mazingira rafiki ya kujiongezea nafasi ya kusajiliwa na timu kubwa,” alisema Mogella.