MABADILIKO ndio wimbo unaoimbwa zaidi kwa sasa pale Yanga. Ni kweli, klabu hiyo imeamua kuachana na mambo ya kizamani na kuchagua maisha mapya. Ni jambo la kupongezwa sana.
Ukitazama namna zoezi hilo linavyoendeshwa hasa huko ‘Instagram’ utadhani ni kama vile linaelekea kukamilika. Huu ndio uongo wanaoishi nao watu wa Yanga kwa sasa. Wanaona kama mchakato wao umepiga hatua kuliko ule wa Simba.
Ni kichekesho. Ukweli mchungu ni kwamba mchakato wa mabadiliko pale Yanga ndio kwanza upo hatua ya awali. Kama ni hatua wamepiga, basi ni kidogo sana. Yaani bado mchakato haujafika hata robo ya ule wa Simba SC. Unajua kwanini? Subiri nitakwambia.
Katika mabadiliko, kuna mgawanyiko wa nyakati. Kuna mwanzo, katikati na mwisho. Mwanzo ni mwepesi sana kama kumsukuma mlevi. Ni sehemu ambayo wengi hupiga hatua kwa haraka.
Ni katika mabadiliko ya katiba ya klabu ili kuruhusu mchakato uanze. Eneo hili tayari Yanga wamekamilisha. Ni eneo ambalo hata Simba walikamilisha kwa wepesi sana.
Eneo la pili ni kuhakiki na kusajili wanachama wapya. Hili ndilo eneo ambalo Yanga wapo kwa sasa. Ubaya ni kwamba wamechukua muda mrefu katika eneo hili. Simba walipita haraka katika hatua hiyo.
Unajua kwanini Yanga wanakwama katika mchakato wa wanachama? Ni kwa sababu wameweka vikwazo vingi.
Kwanza kabisa, wamepunguza faida za wanachama. Hebu fikiria hii leo sio kila mwanachama ana haki ya kuhudhuria mkutano mkuu. Yaani unakuwa mwanachama wa Yanga ili uwe unahudhuria mikutano ya matawi. Inachekesha sana.
Mikutano ya matawi mara nyingi ni kama vijiwe vya kahawa tu. Matawi hayana nguvu yoyote ndani ya klabu. Nguvu kubwa kwa mwanachama ni kupata hiyo haki ya kuhudhuria mkutano mkuu, lakini Yanga wameipoka hiyo nguvu.
Pili, wamepandisha ada ya wanachama mno. Kabla ya mabadiliko, wanachama walikuwa wakilipa Sh1,000 kwa mwezi. Na fedha hiyo angeweza kulipa kwa mwezi mmoja, miezi mitatu ama zaidi. Ajabu ni kwamba kwa sasa Yanga wamepandisha ada hiyo na kuwa Sh2,000. Cha kushangaza zaidi ni kwamba mwanachama anapaswa kulipa ada ya mwaka mzima.
Bado hapo kuna gharama za kadi, hivyo kutakiwa kulipa Sh29,000. Ni Watanzania wangapi wanaweza kulipa ada hiyo kwa mkupuo mmoja? Ni wachache sana.
Watanzania wengi bado wanaishi maisha ya kawaida yaliyo na changamoto nyingi kila siku. Bado hapohapo wanalipa viingilio katika kila mechi. Halafu baada ya hapo unamwambia alipe Sh29,000 ili awe mwanachama. Ni kichekesho kingine.
Hii ndiyo sababu mchakato wa kusajili wanachama pale Yanga umezorota. Licha ya kuweka masharti magumu kuwa ili tawi litambulike lazima liwe na wanachama angalau 100, bado mwenendo sio wa kuvutia. Ila hili hawawezi kulisema hadharani.
Simba walijaribu kufanya ada ya wanachama wao kuwa Sh20,000 zoezi zima likafeli. Wakaacha kimya kimya. Mpaka leo hawajawahi kusema ule mchakato uliishia wapi.
Ukweli mwingine mchungu katika mabadiliko pale Yanga ni eneo la mwisho la kuthaminisha klabu pamoja na kuweka wawekezaji. Bahati mbaya zaidi ni kwamba Yanga imeweka ugumu zaidi katika eneo hili.
Kwanza imeweka masharti ya kuwa na wawekezaji wanne. Yaani wawekezaji hao watagawana asilimia 49 za upande wa pili. Hili jambo ni gumu sana kutekelezeka.
Wakati Simba inatangaza tenda ya kupata mwekezaji, alijitokeza Mohammed Dewji peke yake. Kabla ya kutangazwa kwa tenda, maneno yalikuwa mengi sana. Wanasimba walisema matajiri wengi wanataka kuwekeza klabuni kwao. Walikwenda wapi? Hakuna anayejua mpaka leo.
Sasa Yanga nao wanaishi katika uongo huo huo. Wanaamini kuwa wapo matajiri wengi wanataka kuwekeza klabuni hapo. Ni suala la muda tu kuuona ukweli wake.
Eneo hili la uwekezaji ndio gumu zaidi. Kwanza, ugumu ni kufahamu thamani ya klabu ya Yanga. Wataipimaje thamani yao? Ni kusubiri na kuona.
Pili ni kupata wawekezaji wenyewe. Angalau Simba wakati ule tayari Mo Dewji alishaonyesha nia kabla ya mchakato kuanza. Nani ameonyesha nia pale Yanga mpaka sasa?