BAADA ya kikosi cha Simba kutua nchini kikitokea nchini Benin walikokuwa kwenye mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya ASEC Mimosas, mastaa wa timu hiyo wamepa ni lazima washinde mechi yao ya mwisho na kwenda robo fainali ya mashindano hayo.
Simba inatarajia kucheza na US Gendarmerie ya Niger Aprili 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, mchezo ambao ni lazima Wanamsimbazi washinde ili waende robo fainali. Mchezo uliopita Simba ilichapwa mabao 3-0 mbele ya ASEC ya Ivory Coast.
Meneja wa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema baada ya kurejea nchini juzi Jumanne wakitokea Benin wachezaji walioitwa timu ya taifa wataenda kwenye majukumu na wale ambao hawajaitwa wataenda mapumzikoni.
“Naomba utambue kuwa baada ya kuwasili wachezaji walioitwa timu ya taifa wataenda kwenye majukumu yao na wasiokua na majukumu hayo wataenda mapumziko, ila Machi 27, mwaka huu, kikosi kinarejea kambini kuanza maandalizi ya mechi dhidi ya US Gendarmerie.
“Tunashukuru baada ya mchezo huo kupoteza wachezaji wote wameahidi kupambana katika mechi yetu dhidi ya US Gendamerie, ambapo kila mmoja amejipanga kupata pointi tatu muhimu, kwani siku hiyo mashabiki waje kushuhudia biriani la Caf ambalo limeandaliwa spesho.
Itakumbukwa kuwa, Msemaji wa Yanga, Haji Manara ndiye muanzilishaji wa neno Birinia katika soka la bongo, neno ambalo limekuwa likitumiwa pia na timu mbalimbali.