Home Habari za michezo NABI AIKACHA YANGA …ALA BATA KWA KWENDA MBELE KWAO UBELGIJI…KAZE ASUSIWA...

NABI AIKACHA YANGA …ALA BATA KWA KWENDA MBELE KWAO UBELGIJI…KAZE ASUSIWA KIKOSI…


KOCHA Mkuu wa Yanga, Nabi Mohammed ameanza mapumziko nchini kwao Ubelgiji lakini amechukua tahadhari kubwa. Amesisitiza kwamba ameacha vyuma vyake kikiwemo Fiston Mayele kinajinoa na anaamini mambo yakienda alivyopanga mechi ya Azam itakuwa nyepesi kwake.

Nabi alienda mbali kwa kusisitiza kwamba kila siku atakuwa anafuatilia kujua maendeleo lakini akirejea atakagua ubora wa mchezaji mmoja baada ya mwingine na kama kuna aliyemdanganya kazi anayo.

Akizungumza  akiwa kwake Ubelgiji, Nabi alisema anafanya mawasiliano ya maana na msaidizi wake, Cedrick Kaze juu ya tizi hilo la gym na uwanjani kwa wachezaji waliopo kambini Avic.

Nabi alisema katika ratiba hiyo mapema mara baada ya wachezaji waliosalia kurejea kutoka mapumziko kikosi hicho kitaanzia gym tena kama kawaida.

Kina Mayele wamekiwasha gym ya pale viwanja vya Gymkhana ambako huwa wanafanyia mazoezi yao. Kuanzia jana timu hiyo imerejea na maandalizi mengine ya ufiti wa mwili wakiwa uwanjani sambamba na mazoezi ya mbinu.

Kikosi hicho pia kitakuwa na mchezo wa kirafiki ambao utawahusisha wachezaji ambao hawako kwenye timu za taifa, mechi ambayo itawarudishia ubora wa mechi.

Yanga ina wachezaji 10 pekee ambao hawako kambini ambapo nane kati ya hao wako katika timu za taifa ambao ni kipa Aboutwalib Mshery, mabeki Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Farid Mussa, viungo Feisal Salum na Zawadi Mauya (wote wako Taifa Stars) ,Khalid Aucho (Uganda), Diarra Djigui (Mali) huku Said Ntibazonkiza na Abdallah Shaibu wakiwa na ruhusa maalum wakienda kufunga ndoa.

Nabi alisema kuelekea mchezo wao dhidi ya Azam FC wanahitaji kuwa katika kiwango kikubwa cha ubora ili waweze kuchukua pointi tatu nyingine.

“Siku zote huwa nasema kila mechi kwetu ni fainali ukiangalia ugumu wa mchezo uliopita dhidi ya KMC lakini angalia tunakwenda kwenye mechi nyingine ngumu zaidi dhidi ya Azam,” alisema Nabi ambaye aliwafunga Azam katika mchezo wa kwanza kisha akawapigia mpira mwingi.

“Azam walishinda dhidi ya Namungo ushindi huo unawarudishia nguvu kuelekea mechi yetu, nitakuwa nimesharudi hapo kuungana na wenzangu, muhimu tunatakiwa kuwa katika ubora mkubwa ili tuweze kushinda mechi hiyo.”

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMATATU

AZAM WAJIFUA, SIMBA WALA BATA

Azam wanaendelea kujifua kwenye Uwanja wao wa Chamazi, Dar es Salaam kujiandaa na mechi hiyo ya Yanga na michezo mingine ya Ligi Kuu Bara huku Simba wakiendelea kula bata mitaani kwa likizo fupi waliyopewa.

Simba watarejea kambini Jumapili tayari kwa mechi ya dhidi ya USGN kuwania kufuzu robo-fainali ya Shirikisho Afrika itakayopigwa Dar es Salaam Aprili 3.

Kocha Pablo Franco alisema wakirejea kambini watakuwa na wiki moja ya kukimbiza na ana imani kwamba itatosha kushinda mechi hiyo yenye umuhimu mkubwa kwenye soka la Tanzania.

Uongozi wa Simba umesisitiza kwamba una siku kumi za maandalizi ya kina ya ndani na nje ya uwanja ambayo wanaamini yatawatosha.