Home Habari za michezo HIZI HAPA ‘MASHINE NANE ZA KIMATAIFA’ ZINAZOIPIGANIA HESHIMA YA BENDERA YA TANZANIA…

HIZI HAPA ‘MASHINE NANE ZA KIMATAIFA’ ZINAZOIPIGANIA HESHIMA YA BENDERA YA TANZANIA…


KWA mara ya kwanza kwenye historia ya soka Tanzania, Taifa Stars imekuwa na wachezaji wanane wanaocheza soka nje ya nchi.

Wachezaji hao wameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa na wote walicheza kwenye mechi ya kirafiki iliyo kwenye Kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Jumatano iliyopita ilipoitandika Afrika ya Kati mabao 3-1, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Baadhi walionekana kwa mara ya kwanza kuichezea Timu ya Taifa ya Tanzania, huku wengine wakiwa ni wale waliozoeleka. Wachezaji wote hao waliotoka nje walicheza, sita walianza, wawili wakiingia kipindi cha pili.

Huenda LEO tena wakaonekana wakati timu hiyo itakapocheza tena mechi yake ya pili ya kirafiki ya kimataifa iliyo kwenye Kalenda ya FIFA dhidi ya Sudan.

Huko nyuma, timu ya taifa ya Tanzania haijawahi kuita idadi kubwa kama hii ya wachezaji, wanaosakata kabumbu la kulipwa nje ya nchi kwenye michuano yoyote ile, iwe mechi za kirafiki, Kombe la Chalenji, kufuzu AFCON, au Kombe la Dunia.

Hawa ndiyo wachezaji wanane walioing’arisha Stars ambao waliletwa kutoka nje ya nchi…

#1. Haji Mnoga – Weymouth

Alishawahi kuichezea timu ya Taifa ya England chini ya miaka 17 mwaka 2019. Kwenye mechi ya Jumatano iliyopita dhidi ya Afrika ya Kati, alicheza kama beki wa kulia. Alizaliwa Portsmouth nchini England, timu yake mama ni Portsmouth, lakini anaichezea timu ya madaraja ya nchini, Weymouth kwa mkopo. Haji ana umri wa miaka 19 na kwenye timu ya taifa, Taifa Stars alivaa jezi namba 28. Ameitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi hicho.

#2. Novatus Dismas – Beitar Tel Aviv Bat Yam

Alicheza kama kiungo mkabaji kwenye mechi dhidi ya Afrika ya Kati na kuvaa jezi namba 24. Si mara ya kwanza kuichezea Stars, na anajulikana na mashabiki wengi wa soka nchini, kwani alishazichezea timu za Azam FC, ambayo nayo ilimpeleka kwa mkopo Biashara United hadi ilipomuuza nchini Israel kwa klabu maarufu ya Maccabi Tel Aviv mwaka 2020.

Kwa sasa anaichezea klabu ya Beitar Tel Aviv Bat Yam, akiwa na miaka 19, na ndiye aliyefunga bao la kwanza Jumatano iliyopita dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

#3. Ben Starkie – Spalding United

Mashabiki wa soka Tanzania pia walimwona mchezaji mwingine akiichezea kwa mara ya kwanza Taifa Stars. Huyu ni Ben Starkie ambaye alivaa jezi namba 23. Jina lake kamili ni Ben Antony Swakali akiwa na umri wa miaka 19 kwa sasa.

Huyu pia alizaliwa England, huko Leicester, lakini tofauti yake na Mnoga ambaye aliichezea timu ya Taifa ya England chini ya miaka 17, huku alishaichezea timu ya Tanzania chini ya miaka 20 mwaka jana. Kwenye mechi dhidi ya Afrika ya Kati, alicheza kama kiungo mshambuliaji. Kwa sasa anaichezea Klabu ya Spalding United, ambao inacheza Ligi ya Kanda, Kaskazini mwa England.

SOMA NA HII  AHMED ALLY : NISIWE MNAFIKI...TUNAWAOMBEA YANGA MABAYA ...ADUI MUOMBEE NJAA....

#4. Kelvin John – KRC Genk

Alicheza kama namba tisa kwenye mechi hiyo, ikiwa ni heshima kubwa kwake kupishwa na nahodha wa timu hiyo Mbwana Samatta. Kelvin John ambaye anadai Samatta ndiye aliyemfanya kupambana kucheza soka ili aonekena na yeye aende nje ya nchi, amepata bahati ya kwenda kwenye klabu hiyo ambaye mwenzake ametoka ya KRC Genk. Haitaji maelezo mengi kwani mashabiki wengi wanamfahamu licha ya umri wake mdogo. Hajazunguka sana, ingawa amecheza timu karibuni za umri wote za vijana, kwa sasa yupo kwenye Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji. Jezi yake ni namba tisa.

#5. Abdillahie Yusuph – Yeovil Town

Si mara ya kwanza kwa straika huyu kuicheza Taifa Stars, kwani aliwahi kuitwa mara kadhaa. Naye alianza kwenye kikosi cha Jumatano iliyopita dhidi ya Afrika ya Kati, akivaa jenzi namba 22, akicheza nafasi ya namba 10.

Adi Yusuph kama anavyoitwa, ni mzaliwa na Zanzibar, miaka 30 iliyopita, lakini kwa sasa anaichezea klabu ya Yeovil Town ya nchini England, ambayo kwa mfumo wa soka la nchini humo, ipo daraja la nne.

#6. Mbwana Samatta – Antwerp

Ndiye nahodha ya Taifa Stars. Hahitaji maelezo mengi, mbali ya kumtaja kuwa ni mchezaji wa zamani wa Simba, TP Mazembe, KRC Genk, Aston Villa na Fenerbahce ya Uturuki ambayo ni klabu yake mama, lakini kwa sasa anaichezea Antwerp ya Ubelgiji kwa mkopo, akifunga bao la pili kwenye mechi dhidi ya Afrika ya Kati.

#7. Simon Msuva – Wydad Casablanca

Pamoja na kwamba ana mgogoro na klabu yake, kiasi cha kumfanya arejee nchini na kutocheza kwa muda sasa, lakini haiondoi ukweli kuwa ni mchezaji wa Klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco hadi hapo kesi itakapoisha au FIFA kuamua vinginevyo. Na ndicho kwa asilimia kubwa kimempa hata heshima ya kuitwa kwenye kikosi hicho, aliingia kipindi cha pili kwenye mechi hiyo.

#8. Joshua Mwakasaba – Tusker

Ukiangalia kwenye orodha ya wachezaji wote nane wa Stars, ni wawili tu wanaocheza soka la kulipwa barani Afrika nje ya Tanzania. Ni Msuva na straika huyu ambaye aliingia kipindi cha pili kwenye mechi dhidi ya Afrika ya Kati.

Ameitwa Stars kutoka kwenye Klabu ya Tusker ya Kenya. Ameweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa ndani ya Afrika Mashariki nje ya Tanzania kuitwa. Kabla ya kujiunga na timu hiyo alikuwa kwenye klabu ya Lipuli ya Iringa.