KUNA wakati unajiuliza viongozi wetu wa soka huwa wanafanya maamuzi kwa kufikiria kweli? Ni kama hili la Ibrahim Ajibu kusajiliwa pale Azam FC.
Ni kweli walifikiria ama walimsajili tu kwa kuwa alikuwa sokoni? Simba iliamua kuachana na Ajibu mwishoni mwa mwaka jana baada ya nyota huyo kushindwa kabisa kuonyesha makali yake Msimbazi.
Ajibu alitoka Yanga akiwa staa mkubwa. Simba ikamuwekea fedha ya maana mezani kumrudisha nyumbani. Lakini kwa miaka yote miwili na nusu baada ya kurejea Simba hakufanya chochote cha maana.
Akawa mchezaji wa kawaida. Akakosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza. Baadaye akakosa nafasi katika wachezaji wa akiba. Akawa mchezaji wa mazoezini tu.
Ni kweli, Ajibu ana kipaji kikubwa cha soka lakini siyo mtu anayejitambua sana. Anacheza soka kama vile ana kazi nyingine ya kufanya.
Hana nidhamu ya kazi. Kocha akimkosa anaona kama hampendi. Na ndiyo sababu licha ya kipaji chake kikubwa, hakuwahi kuwa mchezaji wa maana sana.
Wakati Simba imemuuza Clatous Chama kwenda Morocco, iliamini Ajibu anaweza kupata nafasi ya kucheza. Lakini ndio akawa ovyo zaidi. Hadi kina Jimmyson Mwanuke wakaonekana wachezaji wa maana zaidi yake.
Lakini baadhi ya watu wa Azam wakaona anaweza kuongeza kitu katika timu yao. Kweli unataka kushindana na Simba na Yanga kwa kumsajili Ajibu?
Matokeo yake tangu amesajiliwa mpaka leo amecheza michezo mitano tu na kufunga bao moja na hana asisti. Kwa kifupi Ajibu ni mchezaji wa kawaida mwenye jina kubwa.