MASTAA wa zamani wa Yanga, Juma Abdul na Shadrack Nshajigwa wamemsifu kocha Nasreddine Nabi kwa kukiongoza vyema kikosi hicho huku wakiwataka mabeki namba tatu wa timu hiyo kuingia darasani chini ya Farid Mussa.
Mabeki wa kushoto wa Yanga ni Yassin Mustafa, David Bryson na Kibwana Shomari ambaye amehamishwa namba kutoka namba mbili hadi tatu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema usajili uliofanywa na kikosi hicho hasa eneo la beki namba tatu ni mzuri na una tija kikosini lakini matumizi ya namba hiyo kwa kocha Nabi ndio yanawahukumu mastaa hao.
Kocha na mchezaji wa zamani wa Yanga, Nsajigwa alisema mabeki wote waliosajiliwa eneo hilo ni wazuri, wanajua kukaba na kupandisha mashambulizi shida iliyopo kuna vitu wanashindwa kumpa Nabi kutokana na mfumo wake anaoutumia.
“Nimewaangalia wote ni wazuri na ni damu changa lakini kuna vitu anavitaka kocha hawana na ndio maana ameamua kumpa nafasi winga Farid ambaye ameweza kufanya kile anachokitaka kwanza anakaa na mpira mguuni anaweza kufanya kazi nyingi uwanjani,” alisema na kuongeza.
Abdul alisema anavutiwa na kipaji cha Farid hasa akitumika namba tatu anaona mambo mengi mazuri mguuni mwake huku akitumia nafasi hiyo kuwataka wachezaji wanaocheza nafasi hiyo kuhakikisha wanajiongeza.