Home Azam FC KUELEKEA MECHI YA CAF JUMAPILI…SIMBA WAPANIA REKODI YA AS VITA…PAWASA ATOA ONYO….

KUELEKEA MECHI YA CAF JUMAPILI…SIMBA WAPANIA REKODI YA AS VITA…PAWASA ATOA ONYO….


SIMBA ipo kambini ikijifua kujiandaa na pambano  la kufa au kupona la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USGN ya Niger, huku kocha wa timu hiyo, Pablo Franco akisaka heshima na mastaa wakitaka kurejea rekodi waliyoiweka mbele ya Nkana Red Devils ya Zambia na AS Vita ya DR Congo.

Katika mechi hiyo ya Jumapili itakayopigwa kuanzia saa nne usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuna mastaa watano wa Simba watakuwa na kazi ya kuhakikisha inatinga robo fainali kama ilivyokuwa misimu mitatu ya nyuma ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ilipopenya mbele ya Nkana na AS Vita.

Katika nyakati hizo tatu Simba imevuka kibabe kwenda hatua nyingine ikiwamo pambano la kutinga makundi msimu wa 2018-2019 dhidi ya Nkana.

Mastaa Jonas Mkude, Paschal Wawa, Mohamed Hussein, Meddie Kagere na Aishi Manula ni miongoni mwa waliobahatika kucheza michezo yote mitatu kwa mafanikio hivyo uzoefu wao kwenye mashindano hayo unawabeba kufanya kweli Jumapili.

Desemba 23 2018 Simba iliitoa Nkana kwa mabao 3-1 na kutinga makundi Ligi ya Mabingwa baada ya awali kulazwa 2-1 ugenini. Wafungaji katika mchezo huo alikuwa Mkude aliyefunga dakika ya 28 kwa pasi ya Clatous Chama, Meddie Kagere dakika ya 45 kwa kichwa akimalizia krosi ya Nicholas Gyan na Chama akamalia kazi kwa pasi ya Dilunga.

Aliyekuwa kocha wao, Patrick Aussems alianza mchezo huo na Manula, Nicholaus Gyan, Tshabalala, Paschal Wawa, Erasto Nyon, James Kotei, Jonas Mkude, Clatous Chama, Meddie Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi.

Wachezaji wa akiba walikuwa Deogratius Munishi ‘Dida’, Juuko Murshid, Said Ndemla, Hassan Dilunga, Shiza Kichuya, Rashid Juma na Adam Salamba.

Mechi nyingine ni mwaka 2019 Machi 16 Simba ikiifunga AS Vita na kutinga robo fainali – mabao yakifungwa na Tshabalala dakika ya 35, Chama dakika ya 89 akimalizia pasi ya John Bocco.

Aussems katika mchezo huo alianza na Manula, Zana Coulibaly, Tshabalala, Paschal Wawa, James Kotei, Chama, Mzamiru Yassin, Bocco, Kagere na Emmanuel Okwi.

SOMA NA HII  AZAM FC YAONJA JOTO YA JIWE ZANZIBAR

Benchi walikuwepo kina Munishi, Paul Bukaba, Said Ndemla, Dilunga, Haruna Niyonzima, Rashid Juma na Salamba.

Mechi nyingine dhidi ya AS Vita iliyowafumua mabao 4-1 Aprili 3 mwaka 2021 na kutinga robo fainali ilipokutana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na kutolewa katika hatua hiyo kwa jumla ya mabao 4-3. Ikilala ugenini 4-0 na kushinda nyumbani 3-0.

Mabao ya Simba yalifungwa na Luis Miquison dakika ya 29 akimalizia krosi ya Morrison, dakika ya 41 Chama alifunga mabao mawili huku lingine likifungwa na Tshabalala kwa shuti nje ya 18.

Kikosi chini ya Didier Gomes kilikuwa Manula, Morrison, Taddeo Lwanga, Wawa, Chris Mugalu, Miquisson, Shomary Kapombe, Tshabalala, Joash Onyango, Chama na Mkude. Wachezaji wa akiba walikuwa Beno Kakolanya, Rally Bwalya, Kagere, Erasto Nyoni, Dilunga, Francis Kahata na Kennedy Juma.

Akiizungumzia Simba, beki wa zamani wa timu hiyo, Boniface Pawasa alisema imekuwa ikipata ubora mara kwa mra kutokana na namna ambavyo kila mwaka inawakilisha na kucheza na timu kubwa katika michuano hiyo.

“Kila timu ambayo iko katika michuano hiyo ni nzuri na Simba naamini wakitumia vyema nafasi wanasonga mbele kikosi wanacho na hata uwezo pia,” alisema Pawasa.

Kocha Pablo Fraco alinukuliwa waliporejea nchini kutoka Benin walikocheza na Asec Mimosas kwamba, anataka kuweka rekodi ya kuivusha Simba salama ikiwa nyumbani baada ya kukwama kufanya hivyo ugenini walikofumuliwa mabao 3-0. “Nafasi ya Simba kutinga robo fainali ipo. hHata kama mchezo utakuwa mgumu, lakini tunataka kuweka historia mpya,” alisema Pablo.