Wakati Russia ikipanga kujiondoa katika Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), raia wake ambaye ni mmiliki wa Chelsea, bilionea Roman Abramovich imefichuka kuwa alitegewa sumu pamoja na watu wengine wawili wanaoshiriki mazungumzo ya kutafuta suluhu katika sakata la vita kati ya Russia na Ukraine.
Tukio hilo liliripotiwa kufanyika katika mkutano wa majadiliano uliofanyika kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.
Ripoti zinadai kuwa Machi 3, mwaka huu, Abramovich, bilionea mwingine kutoka Russia pamoja na mbunge wa Ukraine, Rustern Umerov walionyesha dalili za kuathirika na sumu ambayo hadi sasa haijajulikana ni nani hasa aliyeratibu jaribio la kuwadhuru.
Inadaiwa kuwa Abramovich na wenzake hao wawili walipoteza uwezo wa kuona na ngozi zao hasa za mikononi zilikuwa zinabanduka, lakini watatu hao walipelekwa Uturuki kwa matibabu ambako afya zao zilirudi katika hali ya kawaida.
Hata hivyo, tukio hilo halikutangazwa hadharani kwa kile kinachotajwa ni kujaribu kulinda usalama wa Abramovich na waathirika wengine wa shambulio hilo.