Kocha Mkuu wa klabu ya Simba Pablo Franco, amesema hawajapata muda mzuri wa kujiandaa na mchezo wa kesho wa Ligi Kuu NBC Premier League dhidi ya Coastal Union utakaopigwa Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga Saa 10 jioni lakini amesema atahakikisha wanashinda mchezo huo.
Kocha Pablo amesema baada ya kumaliza mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Gendarmerie timu ilifanya mazoezi mepesi siku moja na leo kikosi hicho kikiwa jijini Tanga kitafanya mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo wa kesho dhidi ya Coastal Union.
“Ratiba inatubana sana, juzi tumetoka kucheza mechi ngumu ya kimataifa jana tumefanya mazoezi mepesi asubuhi, mchana tukaanza safari ya huku. Tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi’’ amesema kocha Pablo
Kwa upande wa hali ya kikosi kocha huyo raia wa Hispania amesema kuwa nohodha wa kikosi hicho John Bocco hatakuwa sehemu ya mchezo wa kesho baada ya kupata maumivu kwenye maandalizi ya mchezo uliopita dhidi ya US Gendermerie, mchezaji mwingine ni Hassan Dilunga nae ana majeruhi.