Kocha wa Simba, Pablo Franco ameshauriwa kuwa na programu maalumu ya kushambulia kuanzia sasa ambayo itaisaidia kupenya dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini itakayocheza na Wekundu hao Aprili 17.
Wakati akishauriwa hivyo, pia kocha wa Gendarmerie Zakaria Yahaya amesema Simba inaweza kutinga nusu fainali hata fainali za michuano hiyo endapo itarekebisha mapungufu ya safu yao ya ulinzi.
Akizungumza kutoka kwao Niger, Zakaria aliyeshuhudia timu yake ikifungwa na Simba mabao 4-0 jijini Dar katika mechi ya mwisho ya Kundi D ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, alisema Simba ina mabeki bora wa pembeni wanaotamba nyumbani na ugenini, ila kwa Pirates wanatakiwa kuwa na mabadiliko.
“Pirates ina timu nzuri, ina watu ambao wanajua kutumia mapungufu ya kiufundi, wale mabeki wa pembeni wa Simba ni wazuri sana, lakini hawatakiwi kushambulia kama walivyofanya kwetu, niliwaambia hii timu yangu ni changa wachezaji wangu wengi bado hawajakomaa katika mechi kubwa kama hizi na tulifanya makosa sana tulipocheza na Simba huku kwetu,” alisema Zakaria na kuongeza;
“Unapocheza na wachezaji wazoefu na bora kwa mbinu unapopanda kama wanavyopanda wale ni rahisi kuweka mtu pale wanapotoka na wakicheza shambulizi la haraka ni rahisi kukuumiza, huku ilipo Simba sasa ni kwamba ukifanya kosa moja adhabu ni hapo hapo.
“Wanatakiwa kupanda kwa hesabu naamini kocha wa Simba ana akili atawakumbusha hilo ili wasije wakapoteza vibaya katika hizi mechi mbili.”
Akiwazungumzia mabeki wawili wa kati wa Simba alisema hana wasiwasi na ubora wa Henock Baka lakini beki Mkenya Joash Onyango anatakiwa kuandaliwa kiubora zaidi kwa kuwa hata mechi zao mbili hakuwa na ubora mkubwa.
“Shida ambayo naiona kwa Simba ni yule beki wao wa kati anayevaa jezi namba 16 (Onyango) nimemuona mechi mbili sio mtu bora sana ni vile timu yangu inaundwa na wachezaji wasio na uzoefu,” alisema Zakaria na kuongeza;
“Anafanya makosa mengi sana, kwetu amepona lakini zipo timu kila kosa moja wanakuadhibu nafikiri wanatakiwa kumtengeneza vizuri, yule anayetoka Congo (Baka) sina tatizo naye anacheza vizuri.”
Zakaria alisema; “Simba wana wachezaji bora sana kama kule mbele yule anayevaa jezi namba 3 (Morrison), kuna yule aliyevaa jezi namba 7 (Chriss Mugalu) na Pape (Sakho) ni wachezaji bora sana ambao wakati wowote wanaweza kufanya madhara makubwa.”
Naye mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay alisema kuanzia sasa Simba inapaswa kuwa na programu maalumu ya kushambulia mechi yao ya nyumbani ipate angalau ushindi wa 3-0.
Kocha Abdallah Kibadeni alisisitiza Simba iikabili Orlando kwa kushambulia kwa kasi ikitumia ipasavyo kila nafasi kama wanahitaji kusonga mbele ya Wasauzi.